VIONGOZI WA MAKANISA WATOA TAMKO UGIRIKI


Baba Mtakatifu Francisko, Patriaki Bartlomeo wa kwanza na Askofu mkuu Jerome II, wametoa Tamko la Pamoja kuhusu hali ya wakimbizi na wahamiaji kwenye Kisiwa cha Lesvos, Ugiriki. Viongozi hawa wa Makanisa wanapenda kuonesha hofu yao kutokana hali ngumu inayowakabili wahamiaji, wakimbizi na watu wanaoomba hifadhi ya kisiasa Barani Ulaya, wakiwa wanatoka katika maeneo yenye vita, vitendo vinavyotishia maisha ya wengi! Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kufumbia macho hali hii tete ambayo ni matokeo ya uhalifu na vita, dhuluma, nyanyaso za kidini na kikabila; vitendo vinavyowang’oa watu hawa kutoka katika makazi yao. Huu ni uvunjaji wa utu wa binadamu, haki msingi za binadamu na uhuru.
Uhamiaji wa kulazimishwa na ukosefu wa makazi maalum ni hali inayowaathiri mamillioni ya watu na kwamba, hii ni hali tete ya ubinadamu inayohitaji majibu ya mshikamano, huruma, ukarimu na upatikanaji wa rasilimali. Viongozi wa Makanisa kutoka Lesvos, wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kujibu hali hii tete na kilio hiki kwa kushughulikia vyanzo vyake kwa njia kidiplomasia, kisiasa na kwa kutumia huduma ya upendo na kuunganisha nguvu kwa kushirikiana zaidi ili kupata ufumbuzi wa kudumu huko Mashariki ya Kati na Ulaya.
Viongozi wa Makanisa wanasema, wao wanatamani kuona amani ikitawala na kwamba mgogoro huu unapatiwa ufumbuzi wake kwa njia ya mchakato wa majadiliano na upatanisho. Wanatambua mchango ambao umekwishakutolewa kwa ajili ya huduma kwa wahamiaji, wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Wanaomba viongozi wa kisiasa kufanya kila linalowezekana ili watu binafsi, jumuiya pamoja na Wakristo wanabaki katika makazi yao na kuendelea kufurahia haki ya kuishi katika amani na usalama.
Hapa muafaka mpana zaidi wa kimataifa unahitajika sanjari na kuwa na mpango mkakati wa huduma ili kujikita katika utawala wa sheria; kutetea haki msingi za binadamu na makundi madogo madogo ya watu; kusimama kidete kupambana na biashara haramu ya binadamu na magendo; kufunga njia zisizo salama zinazopitia huko Aegean na Ukanda mzima wa Bahari ya Mediterrania, ili hatimaye, kutengeneza mchakato wa makazi salama ya watu! Kwa njia hii, viongozi wa Makanisa wanasema, itakuwa ni rahisi kuweza kuhudumia nchi zile ambazo zinawahudumia watu hawa wenye shida na mahangaiko makubwa.
Viongozi wa Makanisa wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na wananchi wa Ugiriki, licha ya hali ngumu ya uchumi wanayokabiliana nayo, bado wameweza kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na watu wanao omba hifadhi ya kisiasa kwa moyo wa ukarimu na upendo. Viongozi hawa wanaomba kusitishwa kwa vita huko Mashariki ya Kati, ili haki na amani ya kudumu viweze kurejea tena na hivyo kutoa nafasi kwa watu kurejea tena katika makazi yao. Wanaziomba Jumuiya za kidini kuongeza bidii ya kuwapokea, kuwahudumia na kuwalinda wahamiaji kutoka katika dini zote na kwamba, huduma ya upendo iratibiwe kwa kushirikiana na mashirika ya kidini na kiraia. Pale inapooneka kwamba, bado kuna mahitaji, viongozi wa Makanisa wanaziomba nchi mbali mbali kutoa hifadhi ya muda kwa wanaomba hifadhi ya kisiasa na wakimbizi. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba watu wote wenye mapenzi mema watashirikiana kwa dhati ili kumaliza vita inayoendelea huko!
Viongozi wa Makanisa wanakaza kusema katika tamko lao la pamoja kwamba, Bara la Ulaya linakabiliana na hali tete katika utu wa binadamu, ambayo haijawahi kutokea tangu baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia. Ili kuweza kukabilia na hali hii tete, Wakristo wote wanaombwa kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwani hiki ndicho kigezo ambacho kitatumiwa Siku ya Hukumu ya Mwisho.
Viongozi wa Makanisa, huku wakiwa wanapenda kuonesha utii wao kwa Kristo Yesu, wataendeleza mchakato wa kuimarisha Umoja wa Wakristo; Upatanisho na Haki miongoni mwa waamini wao. Makanisa yataendelea kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za wahamiaji, wakimbizi na watu wanao omba hifadhi ya kisiasa; maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Viongozi wa Makanisa wanataka kutekeleza utume wa Kanisa kwa kuwahudumia walimwengu.
Mwishoni, viongozi wa Makanisa wanasema, mkutano wao unapania pamoja na mambo mengine kujenga ujasiri na kutoa matumaini kwa wale wanaokimbia makazi yao na wale wanaowapokea na kuwahudumia. Wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kulinda maisha ya binadamu katika kila hatua; kuibua sera na mikakati inayoambata Jumuiya zote za kidini. Hali mbaya inayoendelea kuwaathiri watu kutokana na hali tete ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na maelfu ya Wakristo inahitaji uwepo wa sala endelevu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI