MAUAJI YA MANABII BADO YANAENDELEA HATA KWA NYAKATI HIZI.


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 11 Aprili 2016 amekemea vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa Sinagogi waliokuwa wanatumia Neno la Mungu kushutumu Neno la Mungu, ili kulinda na kutetea mafao yao binafsi dhidi ya Shemasi Stefano aliyekuwa amejaa neema na uwezo, aliyekuwa akifanya maajabu na ishara kubwa kati ya watu!
Kutokana na wivu wao dhidi ya Shemasi Stefano viongozi wa Sinagogi wakawahamasisha watu kutoa ushahidi wa uwongo dhidi ya Stefano mtu wa Mungu, kiasi hata cha kuhukumiwa kifo! Stefano alishutumiwa kwa kusema kufuru dhidi ya mahali patakatifu, juu ya Torati na Sheria walizopewa na Musa. Baba Mtakatifu anasema mioyo ya watu hawa ilikuwa imegubikwa na giza kiasi hata cha kushindwa kuona ukweli wa Mungu na badala yake wakajikita katika ukweli wa Sheria!
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata Sheria walikuwa wamekwishazipindisha kwa kuwauwa Manabii, jambo ambalo lilikemewa vikali na Yesu mwenyewe, lakini bado waliendelea kuwajengea Manabii minara ya kumbu kumbu, huu ndio ukweli ulioshuhudiwa na wazee wa sheria zilizokuwa zinajikita katika karatasi pasi na ukweli wa mambo; kielelezo cha unafiki, huku wakitaka kujionesha kuwa ni wachamungu mbele ya watu!
Kwa bahati mbaya anakaza kusema Baba Mtakatifu, mioyo yao ilikuwa imefungwa na wala hawakutaka kusikia wala kupokea Ujumbe  na Ukweli wa Neno la Mungu, ambao ni chachu ya hija ya maisha ya Watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema anasikitika sana kusoma ile sehemu ya Injili inayomwonesha Yuda Iskarioti aliyetubu na kuwaendea  waalimu wa Sheria ili kuwarudishia fedha yao, lakini wakashindwa kumpatia nafasi ya kutubu na kuongoka na matokeo yake Yuda Iskarioti akajinyonga hadi kufa! Wakuu wa Sinagogi wakachukua ile fedha ya damu na kuifanyia kazi!
Kwa bahati mbaya viongozi hawa hawakuthamini wala kujali maisha ya mtu wala kuguswa na toba na wongofu uliokuwa umefanywa na Yuda Iskarioti, bali wakaendelea kuonesha shingo ngumu kwa kusimamia sheria zao ambazo walikuwa tayari wamekwishazipindisha, kielelezo cha ugumu wa mioyo! Ni viongozi hawa hawa walioshindwa kupambana na ukweli mfunuliwa kutoka kwa Stefano, wakaenda kutafuta ushahidi wa uwongo, ili kumhukumu na kumtia hatiani! Stefano mtu wa Mungu akahukumiwa kifo kama ilivyokuwa kwa Manabii tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya.
Baba Mtakatifu anasema, historia ya maisha ya mwanadamu inaonesha kwamba, kuna watu ambao wanashutumiwa na hatimaye kuhukumuwa kifo, bila kutenda kosa! Ni watu wanaohukumiwa kwa Neno la Mungu dhidi ya Neno la Mungu lenyewe. Hivi ndivyo watu walivyowatenda Mtakatifu Yohana wa Arco na mashuhuda wengi wa Injili waliochomwa moto huku wakiwa hai dhidi ya Neno la Mungu. Huu ni mfano wa Kristo Yesu aliyekuwa mwaminifu na mtii wa Neno la Mungu, akaishia kutundikwa Msalabani. Anapokuwa njiani na wafuasi wake wa Emmau, anawashutumu kwa uzito wa mioyo yao kutoelewa kile kilichokuwa kimeandikwa kuhusu hatima ya Kristo Masiha na Mkombozi wa ulimwengu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI