Dk. Alberto Gasbarri atunukiwa tuzo ya heshima na Papa Francisko
BABA Mtakatifu Francisko amemtunukia nishani ya heshima ya
utumishi uliotukuka Dk. Alberto Gasbarri, aliyekuwa mratibu wa hija za kitume
za kipapa na mkurugenzi mkuu wa utawala Radio Vatican. Katika hotuba yake, ya
shukrani kwa Dr. Gasbarri, Askofu mkuu Angelo Becciu, katibu mkuu
msaidizi wa Vatican amesema kwamba, nishani hii imetolewa na Baba Mtakatifu kwa
kutambua ukweli na weledi uliomwilishwa na Dr. Gasbarri katika huduma yake
mjini Vatican. Nishani hii ni changamoto ya kusonga mbele ili kuendelea
kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha.
Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kumshukuru kwa namna
ya pekee Dr. Gasbarri aliyekuwa naye karibu katika safari zake. Tukio hili
limeadhimishwa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican.
Itakumbukwa kwamba, Dr. Gasbarri ameitumikia Vatican kwa kipindi cha miaka 47.
Ameng’atuka kutoka madarakani hapo tarehe 1 Machi 2016. Dr. Gasbarri alikuwa ni
mtu maarufu sana, lakini mnyenyekevu, ndiye aliyeratibu hija zote za kichungaji
zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mstaafu Benedikto XVI na Papa
Francisko. Kabla ya kupewa dhamana hii, Dr. Gasbarri alikuwa ni msaidizi mkuu
wa Kardinali Roberto Tucci kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 2005.
Hija za kitume zinazofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni
matukio makuu katika maisha na utume wa Makanisa mahalia. Hiki ni kielelezo cha
umoja, upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni matukio ya Ibadan
a mikutano mbali mbali inayopaswa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa, ili kupata
matunda yanayokusudiwa. Hii ndiyo kazi aliyokuwa anatekeleza Dr. Gasbarri.
Baba Mtakatifu anamshukuru sana Dr. Gasbarri kwa majitoleo na
sadaka yake kwa ajili ya huduma kwa Vatican na Kanisa katika ujumla wake.
Nishani hii ya hali ya juu ni utambuzi wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Dr.
Gasbarri aliyejitoa bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, hija za
kimataifa zinafanikiwa kama ilivyopangwa. Dr. Gasbarri kwenye tukio hili la
kutunukiwa tuzo ya heshima ya hali ya juu, ameongozana na familia yake. Hafla
hii fupi imehudhuriwa pia na viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya
Vatican. Nishani hii ya hali ya juu inayotolewa na Vatican kwa watu maalum
ilianzishwa na Papa Pio IX kunako mwaka 1847.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.
Comments
Post a Comment