Simameni kidete kupambana na rushwa na vitendo vya kigaidi!
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, hivi karibuni limehitimisha
mkutano wake mkuu, kwa kuwataka wananchi wa Nigeria kusimama kidete kupambana
kufa na kupona na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram ambacho kimeendelea kuwa
ni tishio kubwa la usalama, amani, utulivu na maendeleo nchini Nigeria. Umefika
wakati kwa wananchi wa Nigeria kujifunga kibwebwe kupambana na rushwa pamoja na
ufisadi mambo ambayo yanaendekezwa na kundi la watu wachache nchini humo,
wakati ambapo kuna maelfu ya watu wanaoendelea kutumbukia na kuogelea katika
dimbwi la umaskini wa hali na kipato!
Ni wajibu wa Serikali kushirikiana na wadau mbali mbali katika
kufanya maboresho ya hali ya maisha ya wananchi wengi wa Nigeria. Huu ni
ushauri makini ambao umetolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika
mkutano wao mkuu uliohitimishwa hivi karibuni! Vitendo vya kigaidi nchini
Nigeria vimesababisha madhara makubwa katika maisha na maendeleo ya watu,
hususan Kaskazini mwa Nigeria.
Maaskofu wanavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama nchini
Nigeria kwa kuendelea kupambana na Kikundi cha Boko Haram na kamwe wasikate
tamaa, ushindi ni dhahiri, ikiwa kama kutakuwepo na utashi wa kisiasa.
Inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu laki tisa wamepoteza maisha yao na wengine
wengi kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kufanywa na
Boko Haram. Katika kipindi cha miaka kumi na mitano ya vurugu na mashambulizi
ya kigaidi, zaidia ya Wakristo millioni 1. 3 wamelazimika kuyakimbia makazi yao
na leo hii wengi wao wanaishi katika kambi za wakimbizi kana kwamba, hawana
makwao! Jambo ambalo linasikitisha sana!
Maaskofu kutoka Nigeria wanaendelea kusema kwamba, Boko Haram
wamechoma moto na kuharibu Makanisa zaidi elfu kumi na tatu nchini Nigeria.
Wamesababisha hasara kubwa katika maisha ya watu. Uwepo wa Wakristo huko
Kaskazini mwa Nigeria unaendelea kutiliwa mashaka kutokana na mashambulizi ya
mara kwa mara dhidi ya Wakristo. Kuna maeneo mengine idadi ya Wakristo
imeongezeka kwani wale wanaokimbia mashambulizi ya kidaidi wanapata hifadhi
katika maeneo salama.
Changamoto kubwa ni mafungamano ya kijamii yanayotiswa kutokana
na udini usiokuwa na mashiko wala mvuto. Wakristo na Waislam wanapaswa
kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kukuza na kudumisha haki,
amani na maridhiano kati ya watu. Kutokana na changamoto na madhara yote haya,
Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kusimama kidete ili
kuhakikisha kwamba, Boko Haram inashikishwa adabu; utawala wa sheria
unarejeshwa, haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Nigeria
vinadumishwa.
Maaskofu Katoliki Nigeria wanazidi kufafanua kwamba, rushwa ni
adui wa haki na maendeleo ya wengi. Rushwa inaharibu mzizi wa mafungamano ya
kijamii, kiasi cha kuwanyima watu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi;
rushwa inawanyanyasa wanyonge na kuwakweza watu wachache ndani ya jamii.
Mapambano ya rushwa hayana budi kwenda sanjari na maboresho ya maisha ya watu
kwa kupambana na umaskini wa hali na kipato; kwa kuboresha huduma za afya
na elimu, ili hata watoto wa maskini waweze kuona mwanga katika maisha yao.
Mapambano ya rushwa na ufisadi yajengwe kwa kuimarisha misingi
ya usawa, haki na mafao ya wengi. Serikali iwe ni mwelekeo mpana zaidi wa sera
na mikakati yake ya kiuchumi badala ya kutegemea kwa kiasi kikubwa nishati ya
mafuta kama chanzo kikuu cha pato la serikali. Wafanyabiashara wa kati na
wadogo wadogo waendelee kusaidiwa ili kuimarisha shughuli zao za uzalishaji na
utoaji wa huduma.
Maaskofu wanakaza kusema,
maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na Mwaka
wa Upatanisho Barani Afrika, iwe ni nafasi ya toba na wongofu wa ndani; wakati
wa kumwilisha kanuni maadili na utu wema; kwa kuwasaidia watu kiroho na kimwili
pamoja na kujikita katika kutafuta mafao na ustawi wa wengi. Hapa kwa namna ya
pekee, waamini wanahamasishwa: kutubu, kuongoka na kujipatanisha na Mungu
pamoja na jirani zao.
Comments
Post a Comment