Ask.Kilaini:Papa Fransisko ametufungulia mlango wa huruma
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini |
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba
Mhashamu Methodius Kilaini amesema kuwa ndani ya miaka mitatu ya utume wa Baba
Mtakatifu Fransisko Kanisa limeshuhudia jinsi Papa huyo alivyowafungulia
waamini mlngo wa huruma.
Ameeleza hayo hivi karibuni
alipohojiwa na Kiongozi juu ya miaka mitatu ya utume wa Papa Fransisko kama
Halifa wa Mtume Petro, ambapo amebainisha kuwa Papa Fransisko amelifundisha
Kanisa kuwa binadamu hana haki ya kuhukumu bali kusaidia hasa katika kuwaita
watu wenye shida na kuwasaidia.
“Papa Fransisko ametufundisha
kuwa kazi yetu ni kumtafuta mtu yeyote aliyepotea. Ametenda na kufundisha kuwa
kazi yetu ni kutafuta na kumrahisishia binadamu ili aweze kumrudia Mungu. Hivyo
nasi tunakumbushwa kuwa tupo duniani tunapaswa kuisaidia dunia” ameeleza Askofu
Kilaini.
Aidha Askofu Kilaini
ameongeza kuwa mkazo wa Papa Fransisko katika utume wake umejikita katika ‘utu
ndani ya Kanisa’ huku akilenga kuwatafuta wadhambi na kuwarudisha kutafuta uso
wa huruma ya Mungu.
Amesema kuwa kamwe Papa
Fransisko hayuko tayari kuvumilia ubaguzi au kuona wenye dhambi wakitengwa
ndiyo maana daima anatafuta namna ya kuwarudisha binadamu kwa Mungu kwa
kuwapatia fursa mbalimbali.
Ameongeza kuwa moja ya
mafundisho muhimu ya Papa Fransisko ni kuwa hakuna aliye mtakatifu zaidi ya
mwingine, binadamu wote ni sawa na kila mmoja amepewa namna ya kuutafuta
utakatifu.
“Papa Fransisko ametupatia mtazamo
mpya, wa kututaka kuwatafuta wenye dhambi. Mtazamo huu unatupeleka hatua moja
mbele na kutafakari juu ya utu ndani ya Kanisa. Tukiwa hapa duniani anatutaka
tuwatafute wenye dhambi na kuwarudisha kwa Mungu. Ameisaidia dunia katika mambo
mengi ikiwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira, kujali maskini, wakimbizi na
wahamiaji na kutafuta wadhambi” ameongeza.
Masui: Papa ametatua changamoto za uharibifu wa
mazingira kwa vitendo
Kwa upande wake Mkuu wa
Idara ya Caritas Tanzania chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)
Bw. Laurent Masui ameeleza kuwa utume wa Papa Fransisko umeiwezesha dunia
kupata suluhisho lisilo la kinadharia juu ya uharibifu wa mazingira.
Masui ambaye pia ni
mwanaharakati wa mazingira nchini amefafanua kuwa kupitia Waraka wa ‘Laudato Si’
Papa Fransisko ametoa jibu la tatizo la uharibifu wa mazingira, huku waraka huo
pia ukiwa umesaidia uandaaji wa mpango wa maendeleo endelevu ya Milenia.
“Waraka wa Laudato si
umeleta na kuboresha mtazamo unaotekelezeka juu ya kuhifadhi mazingira, na
mtazamo huo umetutoa katika kufikiri kwa nadharia na unatoa dira katika kutunza
mazingira kwa vitendo. Kabla yake kulikuwa na mitazamo tofauti huku kila mmoja
akitaka mtazamo wake uheshimiwe, na katika hilo hakuna aliyetekeleza.
Ni ukweli kuwa Kanisa
linaposema juu ya jambo Fulani linakuwa limetafakari na kupitia mitazamo yote
inayolizunguka jambo hilo kabla ya kutolea maamuzi au ufafanuzi. Hivyo hata
waraka huu umeangalia uhalisia na kutoa mwelekeo unaotekelezeka” ameeleza
Masui.
Akitaja moja ya mambo
muhimu yaliwekewa mkazo katika waraka huo, Bw. Masui ameeleza kuwa Papa
amerekebisha ajenda ya ardhi na kuiweka sawa hasa kwa kusisitiza umuhimu wa
ardhi kwa mtu mmoja mmoja na jamii.
“Waraka huu umegusa watu
wengi hasa kwa jinsi ulivyotoa kipaumbele juu ya umuhimu wa kumiliki ardhi.
Papa amefafanua kuwa ardhi ni makazi, ardhi ni kazi au ajira na ardhi ni
utambulisho wa mtu, hivyo kwa msisitizo huu anataka kutueleza kuwa thamani yetu
na utamaduni wetu upo katika kutunza na kumiliki ardhi” ameongeza.
Aidha Bw. Masui amesema
kuwa Papa Fransisko pia ni mtetezi wa haki za binadamu hasa za wakimbizi na
wahamiaji na mara kadhaa amekuwa akikemea na kushauri makundi mbalimbali na
Jumuiya za Kimataifa kuhakikisha wanawatunza na kuwahifadhi wakimbizi.
Pia Papa ameshiriki
jitihada za kutunza wakimbizi kwa kuagiza sehemu ya Kanisa yenye nafasi
kutumika kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji huku mara kadhaa akitoa barua za
kichungaji wakati wa maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani.
Machi 13, 2016 Baba
Mtakatifu Fransisko ameadhimisha kumbukumbu ya miaka mitati tangu
alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.
Comments
Post a Comment