Papa Fransisko amkumbuka Padri Tom, ataka waliotekwa nyara kuachiwa huru!

Baba Mtakatifu Fransisko mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili tarehe 10 Aprili 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, akiwa bado na matumaini kutoka kwa Kristo Mfufuka aliyaelekeza mawazo na sala yake kwa watu wote waliotekwa nyara katika maeneo yenye vita na kinzani, ili waweze kuachiliwa huru! Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amemkumbuka Padri Tom Uzhunnalil wa Shirika la Wasalesiani aliyetekwa nyara huko Aden nchini Yemen tarehe 4 Machi 2016 na hadi sasa hajulikani mahali alipo!
Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kwamba, nchini Italia, Jumapili tarehe 10 Aprili 2016 wameadhimisha kumbu kumbu ya Siku ya Kitaifa ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambayo imeongozwa na kauli mbiu “Katika Italia ya kesho, hata mimi nimo”! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Chuo kikuu hiki cha Moyo Mtakatifu, kitaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kutoa huduma makini kwa vijana wa kizazi kipya nchini Italia. Chuo hiki kiendelee kutekeleza utume wake katika majiundo kwa kusoma daima alama za nyakati!
Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwasalimia washiriki zaidi ya elfu kumi na sita wa mbio ndefu za Roma kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mbio hizi za kilometa 42 zimewawezesha washiriki kupitia katika maeneo muhimu ya kihistoria yapatayo 500. Mwishoni, amewashukuru waamini na mahujaji wote waliohudhuria kwa wingi kabisa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI