Kuna kilio kikubwa cha ukosefu wa huruma na amani duniani!
Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Jumapili ya huruma ya
Mungu, tarehe 3 Aprili 2015 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican na kuhudhuriwa na umati mkubwa waamini wenye Ibada kwa huruma ya
Mungu. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amesema, Injili ni kitabu cha
huruma ya Mungu ambacho waamini wanapaswa kukisoma na kutafakari yaliyomo!
Injili ya huruma ya Mungu ni kitabu ambacho kiko wazi kinachokumbatia matendo
ya upendo na ushuhuda wa huruma na kwamba, kila mwamini anapaswa kushiriki
kuandika kwenye kurasa za Injili ya huruma kwa kumwilisha matendo ya huruma:
kiroho na kimwili!
Huu ndio mtindo wa maisha ya Kikristo unaowapelekea wengine upendo
na faraja ya Mungu katika maisha yao, kama mwendelezo wa utume uliofanywa na
Kristo kwa kuwashirikisha wafuasi wake waliokuwa na hofu, huruma ya Baba wa
mbinguni na kuwapatia zawadi ya Roho Mtakatifu anayesamehe dhambi na kuwapatia
waamini furaha ya maisha! Mitume wa Yesu, waliogopa, kiasi hata cha kujifungia
ndani, lakini Yesu anawataka watoke huko walikojificha, ili waweze kwenda
ulimwenguni kutangaza ujumbe wa msamaha, mwaliko kwa waamini kujitoa katika
ubinafsi wao, tayari kumkaribisha Yesu!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu kwa njia ya upendo aliweza
kuingia ndani hata pale milango ilipokuwa imefungwa kwa dhambi, kifo na hivyo
kukosa maisha ya uzima wa milele. Yesu anawataka wafuasi wake kufungua malango
ya mioyo yao, tayari kuwatuma kwenda ulimwenguni kutangaza na kushuhudia nguvu
ya upendo wa Mungu inayoponya na kukumbatia. Mbele ya macho ya walimwengu, kuna
binadamu aliyejeruhiwa, mwenye hofu; anayebeba makovu ya machungu ya maisha
pamoja na kukosa uhakika wa maisha.
Kuna kilio kikubwa cha ukosefu wa huruma na amani, kumbe, kama
vile Baba alivyomtuma Yesu, ndivyo waamini pia wanavyotumwa na Yesu
ulimwenguni! Kila ugonjwa unaweza kupata tiba ya huruma ya Mungu, kwani huruma
hii inataka kujimwilisha katika hali ya umaskini; ili kuwaokoa wale wote wanaoendelea
kugandamizwa chini ya kongwa la utumwa mamboleo. Huruma hii inataka kutua
katika donda la kila mwamini, ili iweze kuliganga na kuliponya. Dhana ya kuwa
ni Mitume wa huruma ya Mungu, maana yake ni kugusa na kumfariji Yesu
anayeendelea kujionesha katika miili na nyoyo za watu.
Kwa kutibu na kuganga madonda haya wanamtangaza Yesu aliye hai
na kuwasaidia wengine kuguswa na huruma yake kiasi hata cha kumtambua kuwa ni
Bwana na Mungu kama alivyoungama Mtakatifu Tomaso. Huu ndio utume ambao waamini
wamekabidhiwa. Ni wajibu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa
makini na kuelewa; kwa kuendelea kutangaza na kuandika Injili ya huruma ya
Mungu katika uhalisia wa maisha; kwa kuwatafuta waliopotea kwa uvumilivu na
uwazi kama Wasamaria wema wanaotaka kuonesha ukimya na upendo kwa jirani;
wahudumu wakarimu na wenye furaha wanaopenda upeo bila kudai malipo!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, amani ni zawadi
ambayo Kristo Mfufuka aliwapatia wafuasi wake, ni amani ambayo pia watu wa
nyakati hizi wanaiongojea kwa hamu! Hii ni amani inayobubujika kutoka katika
Moyo Mtakatifu wa Yesu; amani ambayo imeshinda dhambi, kifo na woga! Hii ni
amani inayowaunganisha watu badala ya kuwagawa! Amani inayojikita katika
ukarimu na upendo; amani inayofuta machungu ya maisha na kuwezesha matumaini
kuchipua tena. Amani ni kielelezo cha msamaha unaotolewa na Mwenyezi Mungu,
mwaliko kwa Kanisa kuwa ni chombo cha amani, dhamana ambayo limepewa na Kristo
Mfufuka siku ile Pasaka. Wakristo ni vyombo vya upatanisho, msamaha na
mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu anasema upendo wa
Mungu wadumu milele, ingawa kuna nyakati za majaribu na kukata tamaa, lakini
waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, daima Mwenyezi Mungu yu pamoja nao na kamwe
hawezi kuwaacha pweke! Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa upendo huu usiokuwa
na kifani, anawaalika waamini kuendelea kuchota huruma ya Baba, ili kuwapelekea
walimwengu, lakini kabla ya yote, waamini waombe neema ya kuwa na huruma, ili
kueneza mahali pote nguvu ya Injili!
Comments
Post a Comment