HUDUMA KWA WATU WA MUNGU YASISITIZWA
Hivi karibuni Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini ilifanya mkutano wake wa mwaka kwa kuongozwa na kauli mbiu “Umuhimu wa waamini walei katika maisha ya hadhara katika nchi za Amerika ya Kusini”. Wajumbe hawa wakapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican aliyewataka viongozi wa Kanisa kuhudumia vyema familia ya Mungu kwa kuwaangalia, kuwalinda, kuwasindikiza, kuwaenzi na kuwahudumia kwa kutambua kwamba, viongozi wa Kanisa ni wachungaji wa Kondoo wa Kristo wanaopaswa kuandamana nao katika hija ya maisha!
Baba Mtakatifu katika barua aliyomwandikia Kardinali Marc Armand Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini anawaalika kwa namna ya pekee viongozi wa Kanisa kuwaangalia watu wa Mungu na kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha yao ili kusaidia mchakato wa kuenzi maisha na utume wa waamini hawa kwa kutambua kwamba, huu ni wakati muafaka kwa waamini walei kushika hatamu katika maisha na utume wa Kanisa! Lakini kwa bahati mbaya inaonekana kana kwamba, muda huu umesimama. Wakleri wakumbuke kwamba wanaingia ndani ya Kanisa kwanza kabisa kama waamini walei kwa kupokea sakramenti ya Ubatizo ambayo daima wanapaswa kuionea fahari katika maisha yao kwani ndiyo inayowapatia utambulisho maana kwa kuzaliwa mara pili na kupakwa mafuta ya Roho Mtakatifu, waliobatizwa wanawekwa wakfu kuwa makao ya kiroho ya Roho Mtakatifu na ukuhani mtakatifu na kwamba, waamini walei, wakleri na watawa wanaunda Taifa la Mungu ambalo hali yake ni heshima na uhuru wa watoto wa Mungu, ambao ndani ya mioyo yao Roho Mtakatifu hukaa kama katika Hekalu lake.
Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa makini kwa waamini hawa waliopakwa mafuta na Roho Mtakatifu. Huu ni muda wa kutafakari, kufikiri, kutathimini, kung’amua na kuwa na mwelekeo sahihi juu ya mafundisho yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu “Ukleri” ili kutambua neema ya Sakramenti ya Ubatizo ambayo waamini walei wamepokea na kupigwa chapa ya kudumu katika mioyo yao.
Kumbe, wakleri wasiwe ni kikwazo kwa waamini walei kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika maisha ya hadhara hususan katika maisha ya kisiasa ili kuendeleza moto wa kinabii uliowashwa na Roho Mtakatifu na ambao unapaswa kushuhudiwa na Kanisa zima katika nyoyo za waamini bila kusahau kwamba, mwonekano wa Kanisa kama Sakramenti ni amana ya watu wote wa Mungu na wala si kwa ajili ya watu wachache!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, kuna maeneo ambayo waamini wameweza kuwa mbali kabisa na wakleri katika mchakato wa Uinjilishaji unaojikita katika maisha ya kawaida ya watu, ingawa una athari na mapungufu yake, lakini ukiratibiwa na kudhibitiwa vyema kwa majiundo makini ya Uinjilishaji, una thamani kubwa ambayo inaweza kuzima kiu ya kutaka kukutana na Mungu inayotolewa na waamini wa kawaida kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yanayojikita katika ukarimu na sadaka, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani inayofumbatwa kwa Mungu ambaye ni Baba.
Mungu ni asili na chanzo upendo na uvumilivu ambao unaoneshwa na waamini katika kuubeba Msalaba wa maisha yao, huduma kwa jirani na ibada inayofumbatwa katika maisha ya watu inayomwezesha mwamini kukutana na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Imani ya watu ni dhana ambayo Mwenyeheri Paulo VI aliitumia ili kuonesha msingi, mielekeo, tafiti, hamu na kilio cha ndani kabisa cha watu! Ikiwa kama imani ya watu itasikilizwa na kuratibiwa vyema, watagundua kwamba, hapa kuna uwepo halali wa Roho Mtakatifu anayetenda kazi ndani ya waamini walei wanaosali na kutenda; hali inayojionesha hata katika tamaduni za watu zinazoweza kuwa ni chachu ya Uinjilishaji kwani zinafumbata na kuambata tunu za imani na mshikamano katika haki. Hapa ni jambo muhimu sana kutambua na kuthamini imani ya watu!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, waamini walei wanaishi katika mazingira ambamo utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine unatawala, kiasi hata cha kukosa matumaini; ni watu wanaopambana na maisha ili kuzitegemeza na kuziendeleza familia zao. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwatia moyo, kuwasindikiza na kuwahamasisha kuendelea kuwasha na kushuhudia moto wa imani na matumaini. Viongozi watambue maeneo ya watu wao, tayari kufungua macho ya imani yanayogundua uwepo wa Mungu kati ya watu wake, chachu ya mshikamano, udugu, wema, ukweli na haki.
Mwenyezi Mungu anajifunua kwa wale wote wanaomtafuta kwa moyo mnyofu. Waamini wasaidiwe na kusindikizwa barabara katika maisha yao ya kila siku, ili waweze kushuhudia na kuwajibika vyema katika maisha ya hadhara. Kutokana na changamoto mbali mbali ambazo waamini walei wanakumbana nazo katika maisha na tamaduni mamboleo, wanahitaji kuwa na mifumo mipya ya kuratibu na kuadhimisha imani; kwa kupata nafasi za sala, umoja na mshikamano kwa watu wanaoishi katika maeneo ya mijini. Viongozi wa Kanisa hawawezi kuwa na majibu ya changamoto zote zinazowakumba waamini walei katika maisha yao, kumbe, kuna haja ya kushikamana na waamini kwa kusoma alama za nyakati za uwepo wa Mungu katika maisha ya hadhara.
Baba Mtakatifu anakaza kusema utamadunisho ni mchakato ambao viongozi wa Kanisa wanapaswa kuutumia ili kuwahamasisha waamini walei kuweza kuiishi imani kadiri ya mazingira na watu anaoishi nao; kwa kusoma alama za nyakati, tayari kuishi, kuadhimisha na kushuhudia imani yao; katika furaha na majonzi ya maisha. Utamadunisho ni sanaa inayopania kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kutunza kumbu kumbu ya Kristo Yesu na amana kutoka kwa wahenga, kwani hawa wamesaidia mchakato wa kurithisha imani inayojikita katika sala, upendo na maisha. Familia, Parokia na Shule zimesaidia kukuza na kuendeleza imani ambayo inaendelea kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Waamini walei watunze kumbu kumbu hai ya imani, asili na utambulisho wao unaojikita katika Sakramenti ya Ubatizo, kielelezo cha neema ya Roho Mtakatifu.
Viongozi wa Kanisa wasaidie kuchochea moto wa imani kama walivyofanya mashuhuda mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei ni wadau wakuu katika maisha na utume wa Kanisa na katika ulimwengu katika ujumla wake. Viongozi wa Kanisa wanatumwa kuwahudumia Watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa viongozi wa Kanisa Amerika ya Kusini kwa kuwakumbusha kwamba, wakati wa hija yake ya kitume nchini Mexico amewakumbuka na kuwaombea mbele ya Bikira Maria wa Guadalupe, ili aendelee kulinda na kutunza imani ya watu kama alivyofanya kwa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment