Siku ya Amani na Upatanisho nchini Angola!

Baraza la Maaskofu Katoliki Angola linamshukuru na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 14 tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipokoma nchini Angola. Hii ilikuwa ni tarehe 4 Aprili 2002. Itakumbukwa kwamba, tangu mwaka 1975 Angola walikuwa wanatangwana wao kwa wao na kusahau kwamba, walikuwa ni ndugu wamoja; wagawanywa kwa misimamo ya kisiasa!
Tangu mwaka 2002 nchini Angola tarehe 4 Aprili inaadhimishwa kama Siku ya Amani na Upatanisho! Askofu mkuu Gabriel Mbilingi wa Jimbo kuu la Lubango, Angola, katika maadhimisho haya anasema, Kanisa litaendelea kuchangia katika mchakato wa haki, amani na upatanisho, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi maalum ya Kanisa Barani Afrika. Anasema, amani ni jina jipya la maendeleo, hakuna maendeleo ya kweli pasi na misingi ya haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa.
Askofu mkuu Mbilingi anasema, tarehe 4 Aprili ni siku muhimu sana kwa familia ya Mungu nchini Angola, kwani hata taifa lilianza kuandika ukurasa mpya wa mchakato wa haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa! Huu ukawa ni mwanzo wa mageuzi makubwa ya maisha ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na kidini, ili kujenga ari na moyo wa uzalendo kwa wananchi wote wa Angola. Hii ni dhamana ya kuendeleza kwa namna ya pekee misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.
Ni matumaini ya Askofu mkuu Mbilingi kwamba, familia ya Mungu nchini Angola itaendelea kujikita katika mchakato wa kudumisha amani, utu, umoja na upatanisho wa kitaifa, ili kweli Angola iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi! Lakini wananchi wanakumbushwa kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo amemkabidhi mwanadamu kuitunza, kuiendeleza na kuidumisha! Pale amani inapotoweka, kuitafuta tena, inakuwa ni shughuli pevu!
Umefika wakati kwa familia ya Mungu nchini Angola kuishi kwa amani, upendo na mshikamano, kwani amani iliyoletwa na Kristo Mfufuka inakita mizizi yake kwenye upatanisho. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya toba, wongofu wa ndani pamoja na kuendeleza mchakato wa kuandika Injili ya huruma ya Mungu inayokita mizizi yake na kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI