WOSIA MZITO..USOME
Watu maarufu wanapokata kamba au wanapoondoka hapa ulimwenguni huacha wosia mzito na wengine wanasema wanaacha “nondo za nguvu”. Mathalani katika Biblia Takatifu, Yakobo aliongea na kuacha neno zito kwa watoto wake; Musa aliongea na watu wa taifa lake, kadhalika Samweli na Yoshua walizungumza juu ya Mungu nk. Katika wosia hutolewa ufupisho wa kazi zao, na mipango ya Mungu kwa watu wao ambayo walitegemea kuitekeleza. Katika karamu ya mwisho, Yesu alitoa wosia mrefu unaochukua karibu sura nne za Injili ya Yohane.
Wosia huo ni ushuhuda wa matendo na maneno yake ya mwisho aliyotegemea wafuasi wake wayatekeleze kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Yesu kati yao hadi utimilifu wa dahali. Wosia huo tunausoma baada ya Pasaka unahusu Jumuiyaa yake, yaani lile Kanisa la mwanzo.Yatubidi kusikiliza kwa makini maneno hayo ya mwisho kwani yanatuhusu pia sisi wafuasi wake katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!
Si haba kwamba, hata sisi tunashikirishwa! Wosia huo wa Yesu unatolewa baada ya Yuda kuondoka mezani baada ya chakula cha jioni, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake: Basi huyo akiisha kulipokea tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa usiku. Yuda alipoondoka kulikuwa giza kumaanisha hakukubaliana na jumuiya ile ilikuwa inashabikia mafundisho yahusuyo Mwanga wa upendo, yaani Yesu kujitoa kwa huruma na upendo kwa ajili ya wengine. Kwa vyovyote Yesu alisikitika kwa vile sera zake zilikataliwa. Kadhalika hata sisi tunaweza kusikitika pale tunapoona mmoja wetu au mwana familia anapokataa kuungana na jumuiya au ya familia na kuanza kufanya kivyake au kutokomea mtaani! Hapa hapatoshi kabisa!
Baada ya Yuda kutoka na kuingia gizani, Yesu akaanza kusema: “Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. Kama Mungu ametukuzwa ndani yake, Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake, naye atamtukuza mara.” Angalia, neno hili kutukuza limetokea mara tano katika aya mbili tu. Hapa unaweza kuona Mwana pamoja na Baba wanavyopigiana debe na kupeana ”tough” kwani kazi ijayo si haba wala rahisi, yataka moyo kweli kweli!
Lakini kwa macho ya kibinadamu huko kutukuzana si pahala pake kwa sababu, utukufu tunaomaanisha binadamu ni ule wa kushangiliwa na kupigiwa makofi, wa kuwa pahala pa hadhi ya juu, hapa wengine wanasema, ”hapa watu wanataka kula bata tu, mengine baadaye”. Kumbe, utukufu wa Kristo ni ule wa mtu aliyeshika kikombe cha damu, yaani wa mtu aliyejisadaka kwa ajili ya wengine, mtu anayejisadaka kwa ajili ya huduma inayomwilishwa katika huruma na upendo. Huo ndiyo utukufu wa kweli unaothaminiwa na Mungu. Huu ni utukufu unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo makini cha imani na muungano na Baba wa mbinguni!
Kwa hiyo Yuda Iskarioti anapoondoka na kwenda kufanya mipango ya kumsaliti Yesu, kwa vipande thelathini vya fedha ndiyo wakati muafaka unapodhihirika utukufu wa Kristo. Huu ndiyo utukufu wa kujitoa kimasomaso kwa ajili ya wengine, huo ndiyo udhihirisho wa uso wa huruma ya Mungu ambao ni upendo. Kisha Yesu anawageukia wafuasi waliobaki na kusema: “Enyi watoto wadogo” hapa limetumika neno la Kigiriki teknia ili kuonesha uzao mchanga. Neno hilo teknia linaamanisha pia wanyonge, wadogo, wenye dhambi na wakosefu. Kwa hiyo, katika karamu ya mwisho, Yesu alijitoa mwenyewe katika umbo la mkate na divai kwa ajili ya wanyonge, wadogo, wenye dhambi, wahitaji, wenye njaa na wenye kiu ya haki na uzima wa milele. Maisha yake yaliyotolewa kwa hao teknia yaani watoto wadogo. Hivi kwa kumla na kumnywa Yesu maisha ya wadogo hao yatafanana na maisha yake Yesu. Kwa vyovyote siyo watu wote wanaweza kuukubali ukweli huo, ndiyo maana Yuda aliamua kutoafikiana na sera hii ya Yesu na kuamua kutokomea gizani, huko akakiona kilichomnyoa Kanga manyoya!
Baada ya kuwaita wafuasi wake watoto wadogo na kuwaaga anawaachia zawadi. Kama sisi tungeambiwa kuchagua atuachie zawadi gani, nadhani tungeomba tuachiwe uwezo wa kutenda miujiza. Kumbe, ni kinyume, Yesu anaacha zawadi ya amri tena siyo bora amri bali mpya: “Ninawapa amri mpya.” Kwa kawaida neno mpya kwa kigiriki ni neos. Lakini hapa limetumika neno kainos (mpya) lenye maana ya upya unaofuta vyote vilivyopita, yaani upya uliovunja rekodi. Yakale hayako!
Amri hiyo mpya ni: “Pendaneni kama nilivyowapenda mimi.” Lakini amri hii unaweza kuipinga kuwa siyo mpya kwani inasisitizwa pia katika Agano la kale: Mpende jirani kama wewe mwenyewe. Kumbe, upendo wa Yesu ni amri mpya kwa vile inabidi kubadili fikra na kupenda kama anavyopenda Yesu mwenyewe. Upendo huo wa Yesu ni ule wa kutoa maisha yake kadiri ya mapenzi ya Mungu. Upendo huo ni ushuhuda wa maisha yake mwenyewe, na anataka nasi tulinganishe maisha yetu na maisha yake. Pendani kama mimi nilivyowapenda mimi.
Upendo mwingine wowote ule unaweza kuelekezwa kwa Mungu, lakini upendo aliotuachia Yesu ni upendo wa Mungu uliotimilika katika Yesu. Upendo huo hauna mipaka wala masherti nao ni urithi pekee wa historia na wa maisha aliyotuachia Yesu. Kwa vile hakuna upendo mwingine wowote mkubwa zaidi kama ule wa mtu kutoa maisha yake kwa ajili ya mwingine. Huu ndiyo wosia mkuu aliotuachia Bwana Yesu. Kisha anahitimisha kwa kusema: “Hivyo wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” Kwamba jumuiya inayopokea mapendekezo ya Kristo, itajionesha na kujidhihirisha kwa kupendana. Kwa hiyo maisha ya Yesu unayaona kwenye jumuiya yake katika kupeana chakula, katika kuwahudumia wagonjwa, katika kuwazika wafu, katika kuwatembelea wafungwa, katika kuwasaidia fukara na kuwapa makao wasio na makazi, bila kusahau kuwazika wafu.
Jumuiya namna hiyo huwakilisha umbo la maisha ya Yesu aliyotoa kwa ajili ya wengi. Kuishi Upendo wake ndiyo urithi pekee aliotuachia Yesu na kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu tunaaikwa kuitafuta na kuiambata huruma ya Mungu inayomwilishwa katika huduma ya huruma na mapendo: kiroho na kimwili! Kwa njia hii, tutakuwa kweli tunajitahidi kumuenzi, Yesu ambaye alikuwa ni Mwalimu na Bwana! Lakini akatenda yote kwa unyenyekevu na upendo mkuu!
Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Comments
Post a Comment