DHANA YA VITA IMEPITWA NA WAKATI
Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Chama cha kitume cha Pax Christi kuanzia tarehe 11 – 13 Aprili 2016 linaendesha mkutano wa kimataifa kuhusu Mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu vita na amani sanjari na kuachana na dhana ya “vita halali na ya haki”, ili kujenga na kudumisha kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, ili kupambana na mauaji ya kimbari. Wajumbe wa mkutano huu, wanapembua kwa kina na mapana dhana ya vita mintarafu Maandiko Matakatifu pamoja na kuibua mbinu mkakati utakaofanyiwa kazi ili kuhakikisha kwamba, mafundisho ya Kanisa yanafahamika kwa wadau mbali mbali!
Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua uzito wa mkutano huu na changamoto na madhara ya vita duniani, anasema, mkutano huu unafanyika kwa wakati muafaka, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huruma ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu unaopaswa kukita mizizi yake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu; amani ambayo inakuwa ni chachu ya upatanisho kati ya mwamini na Kristo Yesu. Amani ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Baraza la Kipapa la haki na amani pamoja na Chama cha Kitume cha Pax Christi kwa kuitisha mkutano huu unaowakutanisha watu mbali mbali, ili kupandikiza mbegu ya upatanisho kati ya watu wa mataifa, ili hatimaye, kukuza na kudumisha amani ambayo watu, familia, jamii na mataifa yanajisikia kuwa na haki nayo katika medani mbali mbali za maisha. Kuna haja ya kuendeleza pia mchakato wa amani ya kidiplomasia katika ulimwengu mamboleo, ili kweli haki, amani na uhuru viweze kutawala.
Hapa anasema Baba Mtakatifu, sera na mikakati mbali mbali inayopania kujenga na kudumisha haki na amani kati ya watu inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Mkakati huu unapaswa kwenda sanjari na mchakato wa kuendeleza utamaduni wa kutotumia nguvu na mabavu, mwelekeo chanya dhidi ya vita. Baba Mtakatifu anapenda kwa namna ya pekee kuwashirikisha wajumbe wa mkutano huu, mambo ambayo anapenda kuyapatia kipaumbele cha pekee katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani duniani.
Ni jambo jema kwa binadamu ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itafanikiwa kupiga rufuku vita, hata kama Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikwisha wahi kuzungumzia dhana ya “vita halali na ya haki” inayoweza kuendeshwa na Serikali husika. Jamii ikubali kimsingi kwamba, kuna kinzani katika maisha na kinzani hizi zinapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani. Kanisa linaiangalia Jumuiya ya Kimataifa kama “Familia ya Mataifa”, ndiyo maana Kanisa katika maadhimisho ya kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2016 linaitaka Familia ya Mungu kujenga na kudumisha mahusiano katika maisha ya Jumuiya ya Kimataifa.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kubomoa kuta na utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengi; kuta zinazoendelea kujengwa kwa kisingizio cha usalama, utulivu na amani jamii. Amani ya kweli inaweza kufikiwa kwa kujikita katika mchakato wa huruma kama Baba, mshikamano wa kisiasa; kanuni maadili na mwingiliano wa watu ndani ya jamii. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa ni vita, mwaliko kwa wajenzi na vyombo vya amani kuhakikisha kweli amani inatawala katika akili na mioyo ya watu; kwa kuondokana na utamaduni wa kutengeneza, kulimbikiza na kutumia silaha. Watu wanapaswa kuachana na woga usiokuwa na tija na badala yake kujenga utamaduni wa majadiliano kwa kukubali kutoa na kupokea; daima watu wakiwa wanatafuta ustawi, mafao na maridhiano.
Baba Mtakatifu anasema, tofauti za kitamaduni, mang’amuzi na ujuzi miongoni mwa wajumbe wanaoshiriki mkutano wa haki na amani ni utajiri ambao utawaneemesha washiriki wa mkutano huu, ili hatimaye, kuanzisha mchakato wa ushuhuda wa upyaisho wa kutokutumia nguvu kama silaha makini ya ujenzi wa amani. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa mkutano huu kuendelea kusimama kidete kuunga mkono mapambano ya kufuta adhabu ya kifo duniani; kwa kutoa msamaha sanjari na kufuta deni la nje kwa nchi maskini zaidi duniani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment