Fahamu sheria zinazomlinda mtoto katika Ukristo
KATIKA ukristo kuna amri, sheria, maagizo na hukumu. Sheria inayomhusu
mtoto moja kwa moja iko katika amri kumi za Mungu.
Mtume Paulo anafafanua sheria ya mtoto na wazazi au
walezi wake kutoka katika amri za Mungu pale alipoandika kusema, “Waheshimu
baba na mama yako…” Efeso 6:1. “Enyi watoto watiini wazazi wenu….” “wazazi
wasiwachokoze au wasiwakwaze watoto wasije wakakata tama” Efeso 3:21.
Wajibu wa wazazi kwa watoto
Ukristo unatambua kwamba mtoto ni tunda la ndoa na ni
Baraka katika familia. Hivyo wazazi wana wajibu wa kutambua kuwa kupewa watoto
na Mungu ni Baraka kubwa, kwani kila kitu hutoka kwa Mungu, “…Una kitu gani
wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba
hukukipewa?” (1Kor. 4:7).
Hivyo hata watoto wametoka kwake, “Watoto ni riziki
kutoka kwa Mwenyezi Mungu; watoto ni tuzo lake kwetu sisi” (Zab. 127:3).
Kuwapa watoto wosia mzuri, “Mwanangu, uwe mwaminifu kwa
Bwana Mungu wetu siku zote za maisha yako. Usitende dhambi kwa kusudi, wala
usivunje amri zake. Tenda yaliyo mema maisha yako yote wala usifuate njia ya
uovu. Maana ukitenda vitu kwa uaminifu utafanikiwa katika mambo yako yote…”
(Tob. 4:5-6).
Nidhamu ya kuwalea watoto inasisitizwa sana kwani ndio
msingi wa kujenga taifa bora linalomcha Mungu, “Nanyi akina baba, msiwachukize
watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya kikristo” (Waef. 6:4).
Wazazi wanakumbushwa kuacha hasira katika malezi ya
watoto wao, kwani hasira haijengi bali hubomoa, “Usiwe mwepesi wa hasira maana,
hasira hukaa ndani ya wapumbavu” (Mhu. 7:9). Kadhalika, Mungu anamkumbusha
nabii Yona kuwa hasira haifai, “..unadhani unafanya vema kukasirika?” (Yona
4:4).
Wazazi wana wajibu wa kuwalea na kuwaelekeza watoto wao
mambo yaliyo mema kwa upole, “…lakini sisi tulikuwa wapole kati yenu kama
alivyo mama kwa watoto wake” (1The. 2:7).
Wazazi, walezi na jamii wana wajibu wa kuwasaidia,
kuwajali, kuwatetea watoto yatima, “…tendeni haki, ondoeni udhalimu, walindeni
yatima…” (Is. 1:17).
Wajibu wa watoto kwa wazazi
Kama ulivyo wajibu wa wazazi kwa watoto, vivyo hivyo
watoto nao wana wajibu mkubwa mbele ya Mungu na mbele ya wazazi na jamii.
Wanapaswa kuwa wasikivu, watii na wenye heshima kwa wazazi au walezi wao.
Watoto wanapotimiza wajibu wao vizuri hupata tuzo, Baraka na heri katika maisha
yao.
Katika amri za Mungu, amri ya nne inasema “ waheshimu
baba yako na mama yako ili uishi maisha marefu katika nchi ninayokupa mimi
Mwenyezi Mungu wako” (Kut.20:12)
Utii pia ni kitu muhimu sana kwa watoto kwani unasisitizwa
sana katika maandiko Matakatifu, “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika
Kristo maana hili ni jambo jema” (Waef. 6:1)
Watoto wana wajibu wa kusikiliza na kutekeleza maagizo
wanayopewa na wazazi au walezi kwa wakati. Yesu anaonesha mfano mzuri na wa
kuigwa katika hili, “Basi akarudi pamoja nao hadi Nazareti…” (Lk. 2: 51).
Haki za mtoto katika Ukristo
Ukristo umepinga ukatili kwa watoto katika mambo mengi
kama ifuatavyo:
Ukristo unamtazama mtoto kuanzia mimba (Yeremia 1:4)
(Kutoka 20:13) Amri kumi za Mungu Usiue; hivyo
tunasisitizwa juu ya ulinzi wa mtoto kuanzia mimba.
(Marko 10:13-14) Waacheni watoto wote waje kwangu
msiwazuie, haya ni maneno ya Yesu kuonesha upendo kwa watoto.
(Mithali 22:6) Mfunze mtoto njia njema hataiacha-watoto
warithishwe matendo mema hivyo wazazi ni mfano wa kuigwa
(Yoshua 24:15) kuwalea watoto katika mazingira ya
imani…mimi na nyumba yangu tunamtegemea bwana.
Hivyo ni wajibu wa wakristo kuishi maisha mazuri nay a
mfano katika familia na jumuiya zao, ili kuwafanya watoto waweze kufuata mifano
iliyo bora na mizuri toka kwa wakubwa.
(Imeandaliwa kwa msaada wa ‘mwongozo wa viongozi wa dini
na waamini wao katika kuzuia ukatili dhidi ya mtoto’)
Comments
Post a Comment