UJUMBE WA MEI MOSI
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani inayoadhimishwa Mei, Mosi, 2016 linawataka wadau mbali mbali katika ulimwengu wa wafanyakazi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu hasa wakati huu kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.
Maaskofu katika waraka wao unaoongozwa na kauli mbiu “Kanisa na Jamii” wanagusia kwa namna ya pekee masuala ya haki jamii, haki msingi za binadamu pamoja na athari zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa wafanyakazi kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi ya teknolojia katika shughuli za uzalishaji na huduma za kijamii! Yanagusa: fursa za ajira, mafao ya wengi, ugawaji wa rasilimali na mafungamano ya kijamii.
Mwelekeo wa maendeleo ya teknolojia unaonesha kwamba, baada ya muda si mrefu kazi nyingi ambazo zilikuwa zinatendwa na wafanyakazi, zitaanza kutekelezwa na mashine, hali ambayo italeta mageuzi makubwa katika mchakato mzima wa mtindo wa uzalishaji na ugavi. Katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, maendeleo ya sayansi na teknolojia si lazima yawe ni mbadala kwa kazi ambazo kimsingi zinaweza kutekelezwa na binadamu. Ikiwa kama machine zitapewa kipaumbele cha kwanza, utu na heshima ya binadamu vinaweza kuwekwa rehani na madhara yake ni makubwa kwa jamii husika.
Maaskofu Katoliki Canada wanaitaka Jamii kuwekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa elimu na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kukabiliana na kasi kubwa ya mabadiliko na maendeleo ya sayansi na teknolojia; sanjari na kudumisha utu na heshima ya wafanyakazi dhidi ya madhara wanayoweza kukumbana nayo katika ulimwengu wa kazi.
Rasilimali watu ipewe kipaumbele cha kwanza katika mkakati wa matumizi ya teknolojia ya digitali ambayo kwa sasa inafanya kazi kubwa katika maisha ya mwanadamu. Watu wawe na uhakika wa fursa za ajira na mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia uendelee kusonga mbele pamoja na kuwasaidia wale ambao bado wanasua sua katika hatua hii ya maendeleo! Hapa rasilimali watu ifundwe barabara ili iweze kuwa ni mdau wa kwanza wa maendeleo.
Pili elimu bora na makini ipewe kipaumbele cha kwanza kwa vijana wa kizazi kipya ili waweze kuandaliwa kukabiliana na changamoto, fursa na matatizo wanayoweza kukumbana nayo katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Tatu, ni Jamii isaidie wanafamilia kuthamini na kuendeleza karama na vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili viweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.
Maaskofu wanaendelea kusema, Makampuni mahalia yahamasishwe kutengeneza fursa za ajira kwa vijana na kupewa motisha ili kuzalisha bidhaa na kutoa huduma bora zaidi, huku utu wa binadamu ulindwa na kudumishwa. Mbinu mkakati huu utekelezwe na familia ya Mungu nchini Canada kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake, yaani familia, Serikali, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu na viwanda. Kila mtu achangie kadiri ya uwezo wake, ustawi na maendeleo ya kazi nchini Canada.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment