"UJENZI WA VIZUIZI DHIDI YA WAHAMIAJI/WAKIMBIZI NI UBINAFSI"PAPA FRANCIS
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa Kituo cha Astalli kinachosimamiwa na kuendeshwa na Wayesuiti wa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji mjini Roma, wakati huu kinapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwake, ametumia fursa hii kuomba msamaha kwa wakimbizi na wahamiaji kwa mateso na mahangaiko wanayokumbana nayo kutokana na Jamii kufunga mipaka yake na kutoguswa na mahangaiko yao. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iwe ni fursa ya kuonesha na kushuhudia mshikamano wa huduma ya upendo kwa wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha!
Wakimbizi na wahamiaji imekuwa ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Ulaya kiasi kwamba, baadhi ya nchi zimeamua kuchukua maamuzi ya kufunga mipaka yake, licha ya kushutumiwa na wanachama wengine wa Jumuiya ya Ulaya. Austria ni kati ya nchi ambazo zimeamua kufunga mipaka yake, ili kuzuia wakimbizi wasiingie nchini humo kutoka Italia na Ugiriki.
Msemaji wa Baraza la Makanisa nchini Austria anasema, Makanisa yanatumaini kwamba, Austria itafanya maamuzi yake kwa kuonesha mshikamano katika mchakato wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sanjari na kuendelea kushirikiana na Italia pamoja na Ugiriki ambayo kwa sasa inakabiliwa na wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi.
Bwana Erich Leitenberg, Msemaji mkuu wa Baraza la Makanisa nchini Austria anapinga uamuzi wa Serikali ya Austria kuamua kujenga ukuta mrefu utakaodhibi wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao nchini humo. Ukuta huu unaojengwa huko Brenero, Austria unakuwa ni kielelezo cha kinzani na utengano. Kwa mwelekeo huu mtazamo wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya unagubikwa na giza nene, badala ya kuwa na Ulaya iliyoungana, sasa itakuwa ni Ulaya inayomeguka!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment