Zambia: Kilele cha Jubilei ya Miaka 125 ya Upendo na Huruma ya Mungu
Kanisa Katoliki nchini Zambia, limeadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 125 ya Imani Katoliki nchini humo kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kanisa Katoliki nchini Zambia, miaka 125 ya upendo na huruma ya Mungu” kuanzia tarehe 14-15 Julai, 2017 kwenye Jimbo kuu la Lusaka. Zaidi ya wajumbe 2, 000 kutoka katika majimbo 10 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Zambia wamehudhuria. Hili limekuwa ni tukio la sala na tafakari ya matendo makuu ya Mungu nchini Zambia katika kipindi cha Miaka 125 iliyopita.
Familia ya Mungu nchini Zambia inataka kujizatiti zaidi ili kupambana na changamoto za kiimani zinazoendelea kujitokeza kila kukicha. Inataka kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya familia kwa kuchuchumilia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; inataka kuwa ni chombo cha imani, matumaini na mapendo, kwa kukataa imani za kishirikina ambazo zimekuwa pia ni chanzo cha maafa kwa watu na mali zao! Zambia inataka kujenga na kuimarisha Injili ya imani, matumaini na mapendo; kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano! Tukio hili limepambwa na maonesho mbali mbali kutoka katika Majimbo, Parokia, Taasisi na Vyama vya Kitume. Wadau wakuu katika maadhimisho haya ni vijana ambao wanaonesha ujana wa Kanisa Katoliki nchini Zambia! Miaka 125 si haba na kwamba, vijana wanapaswa kutambua na kuthamini mchango na uwepo wao katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wao ni jeuri ya Kanisa na jamii katika ujumla wake!
Kilele cha maadhimisho haya imekuwa ni Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuuTeresphore Mpundu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Zambia. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Imani Katoliki nchini Zambia yalizinduliwa tarehe 6 Agosti 2016 na tangu wakati huo, familia ya Mungu nchini Zambia imekuwa ikimshukuru Mungu kwa zawadi ya imani; imekuwa ikiomba toba na wongofu wa ndani, kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 125 iliyopita, ili kuomba tena neema na baraka ya kusimama kidete, kulinda, kutangaza na kushuhudia imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake; mambo yanayomwilishwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kielelezo makini cha imani tendaji!
Kauli mbiu ya maadhimisho haya imekuwa ni “Kanisa Katoliki nchini Zambia, miaka 125 ya upendo na huruma ya Mungu”. Huu ni upendo na huruma ya Mungu iliyojionesha kati ya watu wake kuanzia mwaka 1891 hadi mwaka 2016 na sasa wanaendelea kuvuna matunda ya zawadi ya imani wanayopaswa kuishuhudia kwa matendo yenye mvuto na mashiko! Itakumbukwa kwamba, katika ufunguzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Imani nchini Zambia, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, alikwenda Zambia kumwakilisha Baba Mtakatifu Francisko na kuwapatia waamini baraka na matashi mema. Baba Mtakatifu aliwapongeza Maaskofu kwa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo miongoni mwa familia ya Mungu nchini Zambia, akawataka kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, furaha ya Injili inawafikia watu wote nchini Zambia bila ubaguzi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment