Kardinali Pengo: Miaka 25 iliyotukuka
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es
salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya
kuliongoza Jimbo hilo, na kusema kuwa ushirikiano kati yake na waamini ndiyo
uliowezesha mafanikio mbalimbali katika utume wake ikiwa ni pamoja na kuanzisha
Parokia 87.
Katika Misa hiyo ya shukrani
iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu, Kardinali Pengo amewashukuru
waamini kwa sala zao kwa muda wote alipokuwa akipatiwa matibabu, na kusema kuwa
kwa sasa afya yake imeimarika na ameshuhudia makuu ya Mungu.
“Nilipotoka katika chumba cha upasuaji
nilisema maneno haya: ‘Sitakufa bali nitaishi ili niyasimulie matendo makuu ya
Mungu’. Ninawashukuru wanajimbo ambao wameifanya miaka 25 ikamalizika kwa
haraka. Hii inatokana na ukweli kwamba mmoja anatoa amri na wengi wanatenda”
amesema Kardinali Pengo wakati akitoa shukrani kwa waamini.
Akitoa homilia katika misa hiyo Askofu
Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa amesema
kuwa moja ya mambo makubwa yaliyofanywa na Kardinali Pengo katika kipindi cha
miaka 25 ya uongozi jimboni humo ni pamoja na kusogeza huduma karibu na
waamini, ambapo amefanikiwa kuanzisha Parokia 87 na parokia 3 teule.
“Siku zote katika utumishi wake huwa
anaumia akiona waamini wanavuka barabara kwenda kanisani. Ndiyo maana amefanya
kazi kubwa ya kuanzisha parokia 87 na parokia teule 3. Pia katika uongozi wake
mapadri 73 wamepadrishwa. Hii ni changamoto kwenu waamini, hamna budi kuzalisha
mapadri kwani idadi ya parokia alizozianzisha ni kubwa kuliko idadi ya vijana
mliowatoa kuwa mapadri” ameeleza Askofu Nzigilwa.
Adhimisho hilo la Misa Takatifu
limeoongozwa na Kardinali Pengo na kuhudhuria na waamini wa Jimbo Kuu Katoliki
Dar es salaam, ikiwa ni pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin
Mkapa, viongozi wa Halmashauri ya Walei Jimbo na watu wenye mapenzi mema.
Itakumbukwa kuwa Julai 22, 1992
aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mwadhama Laurean
Kardinali Rugambwa alistaafu na moja kwa moja nafasi hiyo ikachukuliwa na
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye kabla ya kuchukua nafasi hiyo alikuwa
Askofu Mkuu mwandamizi wa Dar es salaam (kuanzia Machi, 1990 hadi Julai 22,
1992).
Pamoja na kusherehekea miaka 25 ya
kuliongoza jimbo la Dar es salaam, Kardinali Pengo ameadhimisha miaka 46 ya
upadri na miaka 33 ya uaskofu.
Comments
Post a Comment