Matokeo kidato cha VI: Shule za Kanisa Katoliki
6,495 kati ya 6,840 wafaulu kwenda Vyuo Vikuu
WAKATI Kanisa Katoliki likiwa katika
maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, matokeo ya
kidato cha sita kwa shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki
zimewezesha wanafunzi 6,495 kati ya 6,840 kufaulu na kuwa na sifa za kujiunga
na Vyuo Vikuu.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya
Elimu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Raraiya Alphonce,
imeeleza kuwa jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha sita mwaka
huu ilikuwa 73,692 kitaifa na kati ya hao wanafunzi wa shule za Kanisa Katoliki
waliofanya mtihani huo ni 6,840 sawa sawa na asilimia 9.3%.
Padri Raraiya amesema kuwa wanafunzi
waliofaulu kwa daraja la kwanza ni 1,079, daraja la pili ni 2,852, daraja la
tatu ni 2,564. Ufaulu hafifu, yaani daraja la nne ni 253 na walioshindwa ni 92.
“Ni mategemeo kuwa idadi ya
watakaojiunga na vyuo vikuu kutoka katika shule za Kanisa Katoliki ni 6,495
sawa na asilimia 11.09% ya wanafunzi 58,556 waliofaulu kwa daraja la kwanza
mpaka la tatu. Pongezi nyingi ziwafikie Maaskofu kwa misaada mbalimbali na
miongozo katika kuendesha shule zetu; pongezi kwa Makatibu Elimu Jimbo, wakuu
wa shule husika na walimu wote kwa matokeo haya,” Ameeleza.
Aidha ametoa wito kwa walimu wa shule
hizo kujitathimini na kuona jinsi ya kuendelea kuwasaidia wanafunzi ili wapate
elimu bora. Pia amewaasa Makatibu elimu katika majimbo kuwapatia nafasi walimu
ili wajiendeleza kitaaluma ili wawe walimu mahiri na wenye kuwajibika.
“Matokeo ya mitihani ni kipimo kwetu
sisi walimu kuona ni kwa jinsi gani tumewajibika na kusaidia wanafunzi kusonga
mbele katika kutimiza ndoto zao. Tumshukuru Mungu kwa uwezo aliotupatia wa
kuondoa ujinga ndani ya vichwa na maisha ya vijana wetu. Tuombe neema ya kuwapa
vijana wetu elimu bora na maadili.”
Miongoni mwa shule zilizofanya vizuri
katika matokeo hayo ni pamoja na shule tatu zilizoingia katika nafasi ya kumi
bora (zenye idadi zaidi ya wanafunzi 30) ambazo ni Shule ya Sekondari ya
Wavulana Marian (2), Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian (5), Shule ya Sekondari
Maria Mtakatifu Mazinde (7).
Shule zilizofanya vizuri zilizo na
idadi chini ya wanafunzi 30 ni pamoja na Seminari ya Mt Yakobo- Moshi (4),
Shule ya Sekondari ya Kaisho- Kayanga (7), na Seminari ya Rubya-Bukoba (9).
Kuangalia matokeo yote ingia katika
blogu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: www.tec1956.blogspot.com.
Comments
Post a Comment