RAIS MAGUFULI KUMALIZA TATIZO LA MAJI SEKONDARI GEITA
WANAFUNZI wa Sekondari ya Kristo
Mfalme Nyantakubwa katika Jimbo Katoliki Geita wameandamana hadi mbele ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli wakidai huduma ya maji.
Wanafunzi hao ambao walifika mbele
ya Rais Magufuli eneo la Katunguru akiwa katika msafara wake kwenda kuzindua
mradi mkubwa wa maji Wilayani Sengerema katika kijiji cha Nyamazugo,
waliambatana na walimu wao na mapadri walezi wa shule hiyo huku wakiwa na bango
lenye maandishi “Mhe. Rais Magufuli tunaomba utoe tamko kuhusu kilio chetu cha
maji kijiji cha Nyantakubwa.”
Akizungumza na blog hii, Mkuu wa
shule hiyo ya Sekondari ya wasichana ya Nyantakubwa padri George Nkombolwa
amesema wamefikia uamuzi wa kwenda mbele ya Rais kufuatia kutelekezwa kwa Mradi
wa maji wa vijiji vya Chamabanda Nyantakubwa, Nyamtelela na Kasungamile huku
viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wakikaa kimya.
“Tatizo la maji ni kubwa sana
kijijini Nyantakubwa na hasa kuendesha shule bila maji ni gharama kubwa
sana. Tunasikitika hatuoni hatua zozote na mradi una karibuni miaka 5, hakuna
matumaini,” amesema padri George.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya
wilaya ya Sengerema Magesa Mafuru alipotembelea shuleni hapo alisema kuwa mradi
huo wa maji ulikwama baada ya Mkandarasi aliyekuwepo kushindwa kazi na hivyo
wamemuuzia mkandarasi mwingine atakayekamilisha kazi hiyo, lakini hakuna
kinachofanyika.
Akizungumzia tatizo hilo Rais John Magufuli
wakati wa hotuba yake kijijini Katunguru ameomba wananchi kuwa na subira kwani
Serikali inafanyia kazi miradi mingi ya maji na kwamba yote haiwezi kuisha kwa
siku moja.
“Tunafanyia kazi miradi mingi sana
ya maji na tunafanikiwa. Lakini hatuwezi kukamilisha yote kwa siku moja...kwani
hata Mungu aliumba hatua kwa hatua kwa siku sita na ya saba akapumzika.”
Wakati huo huo, Raisi John Magufuli
amempongeza Paroko wa Parokia ya Nyantakubwa Jimboni Geita, padri George
Nkombolwa kwa kutoa huduma nzuri ya elimu kwa wasichana.
Raisi amempongeza padri George
wakati akiongea na wananchi wa Kijiji cha Katunguru akiwa njiani kwenda
kuzindua mradi wa maji wilayani Sengerema.
“Nakupongeza sana Baba Paroko kwa
kuelimisha wasichana. Ninyi wasichana someni kwa bidii na muache kudanganywa
eti ËŠnakupenda`, acheni mambo hayo hadi mhitimu masomo. Naendelea kukazia
tena..mtoto wa kike awe shule ya Msingi au Sekondari akipata mimba ndiyo basi
hatarudi tena shuleni. Ataenda huko awe mzazi na wazazi wenzake.” Rais
amesema.
Mhe. Rais amesema pia kuwa kwa
upande wa wavulana au wanaume watakaowapa mimba wanafunzi wajue kuwa miaka 30
inawasubiri jela.
Habari
ambazo zimeifikia blog hii
ni kuwa baada ya ziara ya Rais Magufuli kukamilika na kuelekea Wilayani Chato,
Mhandisi wa maji Wilaya ya Sengerema Bw. Blaise amefika katika Shule ya
Sekondari Yesu Kristo Mfalme Nyantakubwa siku ya Jumatano na kuahidi kuwa
mkandarasi mpya amekwishapatikana na akaahidi kuwa maji yataanza kutoka baada
ya miezi 6.
Comments
Post a Comment