VIWAWA SUMBAWANGA WAMWOMBEA KARDINALI PENGO
Vijana wa Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki Sumbawanga wamefanya
maadhimisho ya misa ya kumuombea kwa
Mwenyezi Mungu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo azidi kuimarika katika afya yake ili aweze kuendelea na wajibu wake wa utume.
Maombi hayo yamefanyika wakati wa Kongamano
la vijana Jimbo Katoliki Sumbawanga lililojumuisha jumla ya vijana 408 kutoka
parokia 21 za Jimbo Katoliki Sumbawanga lililofanyika kwa siku 5 na
kuhitimishwa dominika ya moyo mtakatifu wa Yesu parokiani Mwazye sehemu ambapo
alizaliwa Kadinali Pengo.
Akiongoza mamia ya vijana katika Kongamano
hilo, Mkurugenzi Idara ya vijana Jimbo Katoliki Sumbawanga padri Christopher
Mayemba amewapongeza vijana kwa uamuzi wao huo wa kujali na kuthamini wazee na
hasa viongozi wa Kanisa katika mwaka huu wa Jubilei ya miaka 100 ya upadri
kwani kunaonesha kujali na kuthamini shughuli za kichungaji zinazofanywa na
Askofu Mkuu huyo.
“Ninawapongeza sana wapendwa vijana
katika misa hii kwa kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Kardinali Pengo ambaye hivi
karibuni amerejea nchini kutokea kwenye matibabu, hivyo Mwenyezi Mungu amjalie
nguvu na afya njema ya mwili na roho aweze kuimarika na kuendeleza utume. Mmefanya
kitu chema na hasa kwa mwaka huu ambapo Kanisa la Tanzania linafanya Jubilei ya
miaka 100 ya upadri, basi mzidi kuwaombea mapadri na kuwasaidia waweze kufanya
utume wao wa kuliongoza Kanisa kwa sifa na utukufu wa Mungu,” amesema padri Mayemba.
Akieleza malengo ya Kongamano hilo kwa
vijana kwa mwaka huu wa Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo na miaka 100 ya upadri
kufanyika katika parokia ya Mwazye, Katibu Mtendaji Idara ya Vijana Jimbo Bw.
Emanuel Mathias amesema kuwa parokia ya Mwazye ina historia ya pekee katika Kanisa
na hasa Jimbo Sumbawanga kwa kuzaa miito
mitakatifu ya utawa na upadri na zaidi kutoa maaskofu wawili ambao wanaendelea
kulitumikia Kanisa akiwepo Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus
Sangu na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es
Salaam ambao wamezaliwa katika parokia hiyo.
“Mbali ya zawadi hii ya miito
mitakatifu jimboni Sumbawanga na Taifa kwa ujumla ni jukumu letu pia kuwaombea
viongozi wetu wazawa wa parokia hii na
hasa Kadinali ambaye amerejea kutoka kwenye matibabu hivi karibuni, wito wetu
pia ni kwa viwawa wenzetu Tanzania kuungana nasi katika kumuombea ili Mwenyezi Mungu
aweze kumjalia afya njema azidi kuchunga kondoo wake na hasa vijana ambao ndilo
Kanisa la kesho.”
Kongamano hilo la vijana hufanyika
kila mwaka jimboni Sumbawanga ambapo huhusisha parokia 21 zinazounda Kanda 4
ambazo ni Kanda ya Kati inayoundwa na parokia za Kanisa Kuu, Kristo Mfalme,
Roho Mtakatifu, Mt. Fransisko wa Asizi, Ipito, Izimba na parokia ya Familia Takatifu.
Kanda ya Kusini inayoundwa na parokia za Tunduma, Laela, Mpui, Kaengesa na
parokia ya Mwazye. Kanda ya Kalambo inayoundwa na parokia za Ulumu, Matai, Sopa
na Kasanga pamoja na Kanda ya Nkasi inayoundwa na parokia za Chala, Namanyere, Kirando na parokia ya Kala.
Comments
Post a Comment