Kilele Jubilei miaka 100 upadri Tz
Zaidi ya 3000 kushiriki Dodoma
IMEELEZWA kuwa zaidi ya mapadri 1000, walei
1000 na watawa 1000 wanatarajiwa kushiriki maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya
Miaka 100 ya Upadri Tanzania, yanayotarajiwa kufanyika katika Jimbo Kuu
Katoliki Dodoma mnamo Agosti 15, 2017.
Akiongea na Kiongozi hivi karibuni,
Katibu wa Umoja wa Mapadri Tanzania (UMAWATA) Padri Jovitus Mwijage ametoa wito
kwa mapadri, watawa na walei kujitokeza na kuthibitisha ushiriki wao katika
maadhimisho hayo, kwa kulipia mchango wa shilingi 200,000/= ambapo itawawezesha
kushiriki kilele hicho kuanzia Agosti 13 hadi 16.
Akielezea ratiba ya maadhimisho hayo,
Padri Mwijage amesema kuwa washiriki wanatarajiwa kuwasili Dodoma Agosti 13
ambapo Misa ya ufunguzi itafanyika Agosti 14 kuanzia saa 2 asubuhi katika
Kanisa Kuu la jimbo. Baada ya Misa Takatifu washiriki watapata fursa ya
kushiriki semina ambapo mapadri watakuwa katika eneo lao huku waamini na watawa
nao wakipatiwa semina hiyo katika eneo jingine.
“Semina ya kwanza kwa mapadri itatolewa
na Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Desderius Rwoma, na mada inasema
‘Sababu zinazoweza kusaidia upatikanaji wa miito kwa haraka. Mada ya pili
itahusu ‘baada ya miaka 100 ya upadri, maisha yetu ya kiroho, mahusiano yetu
kama mapadri na utume wetu uweje’ na mada hii itatolewa na Padri Titus Amigu”
amesema.
Ameongeza kuwa katika kuelekea kilele
hicho mapadri katika majimbo mbalimbali nchini wameshiriki katika kuzindua
jubilei hiyo kijimbo pamoja na hija zilizolenga kuwaimarisha mapadri hao.
Amesema kuwa Januari 24 hadi 28, 2017 mapadri walihudhuria semina iliyofanyika
katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambapo majimbo mbalimbali
yalituma wawakilishi.
“Lengo la semina na hija mbalimbali
zilizofanyika ni kupyaisha utume wa mapadri baada ya miaka 100 ya upadri.
Tulifanya pia semina ya wakufunzi wa seminari za jimbo ambayo iliwakutanisha
magombera wa seminari kubwa na ndogo na baadhi ya wakufunzi na wakurugenzi wa
miito majimboni” amesema.
Pia ameeleza kuwa yeyote anayehitaji
kushiriki maadhimisho hayo huko Dodoma anapaswa kutuma fedha za mchango na jina
lake kwenye akaunti za UMAWATA au kwa kuwasiliana na wenyeviti wa umoja huo
walioko majimboni au kwa kupiga namba 0765746644.
Comments
Post a Comment