‘Anayemtangaza Mungu hawezi kusambaza habari mbaya’ Ask Nzigilwa
KANISA linapojiandaa kuadhimisha Siku ya
Upashanaji Habari, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam amesema
kuwa jamii inayofurahia kusambaza habari mbaya kamwe haimtangazi Mungu. Amesema
hayo hivi karibuni katika Misa ya shukrani kwa jubilei ya miaka 25 ya Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo, tangu aliongoze jimbo hilo.
Askofu Nzigilwa amesema kuwa waamini
hawana budi kupokea habari njema na kuzipeleka kwa watu, licha ya ukweli kwamba
habari njema huwa hazipendwi na watu.
“Watu wanapenda kusikia habari za ovyo.
Kutopenda habari njema ni kikwazo katika kumtangaza Mungu, hivyo kila mmoja awe
msaada katika uinjilishaji na siyo kuwa kikwazo. Pia msiwe sababu ya watu
kuumia wanapoleta habari njema, kabla ya kuitangaza habari njema tuwe tayari
kuipokea kwanza” ameeleza.
Kanisa linajiandaa kuadhimisha siku ya
upashanaji habari hapo Agosti 6, ambapo Kurugenzi ya Mawasiliano Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) itaadhimisha siku hiyo kwa Misa Takatifu,
maonyesho ya kazi inazozifanya na kisha mada mbalimbali, ambapo maadhimisho
hayo yanatarajiwa kufanyika TEC Kurasini jijini Dar es salaam.
Baadhi ya kazi zitakazoonyeshwa katika
maadhimisho hayo ni pamoja na studio mpya na ya kisasa inayotarajiwa kuanza
kukodishwa kwa ajili ya kuzalisha vipindi mbalimbali, uzalishaji wa gazeti la
Kiongozi, uchapishaji wa vijarida, kalenda, kadi na ubunifu unaofanywa katika
kitengo cha usanifu.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Fransisko
katika maadhimisho ya siku ya Upashanaji Habari unaongozwa na kauli mbiu
“Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe” (Is 43:5), ambapo ametoa wito kwa
vyombo vya habari kutangaza habari za matumaini na imani badala ya kujikita
katika kutangaza habari mbaya, za ovyo na zenye kukatisha tamaa.
Comments
Post a Comment