Jamii yaaswa kuwathamini watoto yatima
MKURUGENZI wa utume wa Walei Jimbo Katoliki
Mbeya na vyama vya Mashirika na Jumuiya za Kitume Jimbo, Padri Sirilo Mwalyoyo
ameyaalika Mashirika na wadau
mbalimbali wa masuala ya kijamii
kushirikiana na Serikali katika kuwalinda na kutetea haki za watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ili waweze kukua katika malezi na maadili mema.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea
kituo cha watoto yatima cha Aman kilichopo Kata ya Nsalaga jijini Mbeya,
ziara iliyoratibiwa na Shirika lisilo la
kiserikali la Sauti ya Mama Afrika(SAMAFO) na watu wenye mapenzi mema, padri
Mwalyoyo amesema kuwa binadamu
wanapoteza dhana ya utu na hivyo kuwasihi wasamaria wema kuwajali, kuwasaidia na kuwaendeleza watoto yatima ili waweze kujisikia kuwa nao
ni binadamu kama walivyo wengine.
“Watu ambao hawana usaidizi wa karibu
wanayo haki ya kuishi, na kwa vile hawana haki ya kujitetea basi wale wanaowalinda waweze kuwatetea na
kuwalinda dhidi ya ukatili wa aina yoyote
ile na hatimaye waweze kuwa na faida kwa jamii na Taifa.”
Padri Mwalyoyo amefafanua kuwa
watoto yatima ni jamii
inayohitaji msaada katika nyanja mbalimbali za makuzi mathalani mavazi mazuri,
malazi mazuri, elimu na afya na kwamba jukumu hili ni vyema libebwe kwa ukaribu na watu wenye nafasi badala ya
kuiachia Serikali, makanisa na misikiti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa SAMAFO, Tabitha Bughali ameiomba Serikali iwapatie uwanja watakaojenga nyumba ya amani ambayo lengo kuu ni kuwahifadhi na
kuwakutanisha wanawake, vijana na watoto
wanaofanyiwa vitendo vya ukatili katika jamii wanazoishi na vyombo vya ulinzi
na usalama ikiwemo misaada ya kisheria.
Aidha amewaonya watoto hao
kutojihusisha na masuala ya anasa za kidunia
ambazo mwisho wake zitawasababisha kupoteza maisha, kufanyiwa ukatili,
kupewa mimba na kutelekezwa na mwisho kuzitoa ama kutupa watoto huku akiwasihi
watoto hao kuwa watakapomuona mwenzao anakengeuka basi walindane wenyewe
kwa wenyewe kwa kutoa taarifa kwa wasimamizi wa kituo ama wamtafute na kumshirikisha
yeye.
Msimamizi wa kituo hicho, Bahati Pangani amewashukuru wasamaria wema kuwatembelea, kufurahi na kula
nao pamoja ikiwemo na kuwapatia mahitaji
mbalimbali kwani ndicho kitu pekee wanachokihitaji katika maisha yao na
kwamba kwa mujibu wa maelekezo wa
Serikali watoto hao wanaishi katika
jamii zao na kukutana walau mara
mbili kwa wiki katika siku za Jumamosi
na Jumapili.
Hata
hivyo mmoja wa wahudumu wa kujitolea kutoka nchini Uswisi, Anna
Sprecher ameelezea furaha yake baada ya kuiona jamii ya kitanzania inavyowajali
watoto yatima, kuwatembelea na kuwapatia misaada mbalimbali ikiwemo ya kielimu
na kisheria ambayo itawasaidia katika
maisha yao ya baadaye na hatimaye kuwakumbuka yatima wenzao pia.
Comments
Post a Comment