HAKI ZA WAFANYAKAZI ZITETEWE
Kuna haja ya kukuza na kudumisha mafungamano ya kijamii katika masuala ya kazi na ajira, ili kuwalinda na kuwategemeza wazee sanjari na kuwapatia vijana fursa za ajira, ili waweze kuitekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu zaidi. Utu na heshima ya binadamu ni mambo msingi msingi katika mchakato mzima wa ukuaji wa uchumi na kwamba, kazi na mfanyakazi ni sawa na chanda na pete, ni mambo yanayokwenda pamoja na kukamilishana. Bila fursa za ajira, maisha yanakuwa magumu kupita maelezo na kazi bila utu ni utumwa na nyanyaso! Fursa ya ajira ni mfumo wa hali ya juu kabisa wa ushirikiano kati ya watu ambao umewahi kutengenezwa katika historia ya maisha ya binadamu. Kuna mamilioni ya watu wanashirikiana kwa kufanya kazi na hivyo kusaidia kusongesha mbele gurudumu la maendeleo, ustawi na mafao ya wengi!
Mwanadamu ameumbwa mwili na roho, anapaswa pia kujengewa utamaduni wa kupumzika baada ya kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa, ili kujichotea nguvu tena! Huu ndio utamaduni wa mapumziko, unaomwezesha mfanyakazi kuweza kujisadaka pia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia yake; kushiriki katika ibada mbali mbali na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Watoto kamwe wasifanyishwe kazi kwani zinawadumaza katika malezi na makuzi yao. Wagonjwa wana haki ya kupata tiba na mapumziko.
Pamoja na yote haya, bado kuna jeshi kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira; watu ambao pengine katika maisha yao yote, hawataweza kupata ajira kutokana na sababu mbali mbali. Kuna haja kwa jamii kuangalia mapato ya akiba ya uzeeni ili yaweze kuwa na usawa ndani ya jamii! Inasikitisha kuona kwamba, kuna watu wanakula “pensheni iliyonona” wakati ambapo, kuna watu wengine wanachechemea kwa “pensheni iliyokondeana” utadhani imekosa lishe bora! Inasikitisha kuona kwamba, wazee wanafanyishwa kazi kwa muda mrefu sana, wakati kuna vijana wa kizazi kipya ambao hawana fursa za ajira. Ikumbukwe kwamba, vijana ni chachu ya ari na moyo mkuu wa kufanya kazi; wao ni nguvu kazi ilisiyokuwa na mbadala; ni cheche za furaha na matumaini ya maisha na kikolezo kikuu cha ustawi na maendeleo ya wengi.
Kutokana na upembuzi huu yakinifu, kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya wa ujenzi wa jamii ya binadamu unaofumbatwa katika mshikamano wa kijamii katika kazi, ili kutoa nafuu ya kazi kwa wazee wanaojiandaa kwenda kula pensheni, ili nafasi yao, iweze kuendelezwa na vijana wa kizazi kipya kwa ari na moyo mkuu. Kwa mwelekeo huu, wazee wanakuwa ni amana na rejea katika masuala msingi ya maisha na mafungamano ya kijamii.
Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 28 Juni 2017 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho na Vyama vya Wafanyakazi nchini Italia, Cisl. Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu mawili yaani: Unabii na Ugunduzi muhimu sana katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Vyama vya wafanyakazi vinapaswa kutekeleza dhamana na utume wake wa kuwa ni sauti ya kinabii, inayoweza kukemea dhuluma, nyanyaso na ukosefu wa haki msingi za wafanyakazi. Viongozi wake wawe ni sauti kwa watu wasiokuwa na sauti kama ilivyo katika Maandiko Matakatifu. Nabii Amosi anasikitishwa sana na makosa matatu ya Israeli na kwamba, kutokana na makosa haya lazima wapate adhabu kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha na maskini kwa jozi ya viatu na wamepotosha njia ya wenye upole.
Leo hii kuna haki msingi za wafanyakazi zinazobezwa na waajiri, lakini tabia ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi ni kutaka kufumbia macho ukosefu wa haki msingi za wafanyakazi! Matokeo yake, wanajiangalia wenyewe kiasi cha kugeuka kuwa kama vyama vya kisiasa, kwa lugha na mtindo wao wa maisha. Umefika wakati kwa viongozi wa wafanyakazi kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wafanyakazi.
Pili, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kukuza na kudumisha kipaji cha ugunduzi katika maeneo ya kazi; kwa kulinda fursa za ajira kwa wale walionazo ili kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mchakato wa uzalishaji na utoaji wa huduma hayawapokonyi fursa za ajira kwa wafanyakazi, hali ambao itagumisha maisha ya wafanyakazi wengi zaidi. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yawasaidie vijana wa kizazi kipya kupata fursa za ajira zinazopaswa kulindwa na kutegemezwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi.
Mchakato mzima wa uzalishaji na huduma hauna budi kuzingatia mafungamano ya kijamii, mwelekeo ambao unaendelea kutoweka kila kukicha kutokana na kukithiri mfumo wa ubepari. Soko huria limekuwa ni chanzo kikuu cha kutoweka kwa haki msingi za wafanyakazi, ambao wanageuzwa kuwa kama bidhaa sokoni. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 40% ya vijana wenye umri wa miaka 25 na kuendelea hawana fursa za ajira nchini Italia. Vyama vya wafanyakazi vinapaswa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea vijana hawa ili waweze kupata fursa za ajira. Lakini kwa sasa vita ya fursa za ajira ni kati ya wakimbizi na wahamiaji; na kati ya maskini na maskini!
Changamoto kubwa ni rushwa inayofifisha haki msingi za wafanyakazi. Rushwa na ufisadi vinaanza kuwapekenyua hata viongozi wa vyama vya wafanyakazi, kiasi hata cha kuamua kufumbia macho changamoto ambazo walipaswa kuzivalia njuga anasema Baba Mtakatifu Francisko. Wanawake wamekuwa wakipunjika sana katika masuala ya malipo kiasi cha kuonekana kuwa kama ni wafanyakazi kundi la pili hata kama wana sifa, ujuzi na weledi ule ule kama walionao wafanyakazi wenzao wanaume. Tatizo hapa ni kuendekeza sera na siasa za mfumo dume ambao umepitwa na wakati. Wanawake wapewe haki zao msingi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa wafanyakazi kujielekeza zaidi katika mambo msingi ya wafanyakazi, ili kujenga jamii inayoheshimiana na kujaliana wakati wa raha na shida!
Viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanapaswa kutambua kwamba, wao ni msingi wa jamii katika kutafuta, kupigania na kudumisha haki msingi za wafanyakazi. Baba Mtakatifu anasema, mzizi neno wa “Sindaco” ni kutoka katika lugha ya Kigriki “Syn-dike” yaani “haki ya pamoja”. Haki inaweza kutendeka, ikiwa kama uchumi utafumbata sera na kanuni shirikishi, ili kusiwepo na mtu anayetengwa katika mchakato mzima wa uzalishaji na utoaji wa huduma duniani. Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi, kuongoka, ili kuanza kujikita katika masuala msingi ya haki za wafanyakazi, kila mtu akijitahidi kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment