Tumieni vipaji vyenu kwa faida-Askofu Ruzoka asisitiza
ASkofu
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora Mhashamu Paulo Ruzoka amewataka waamini wote
kujitegemeza kwa Mwenyezi Mungu katika kutumia vipaji vyao kwa faida ya wote
popote walipo bila majivuno.
Rai hiyo ameitoa hivi karibuni katika Misa Takatifu
aliyoiadhimisha katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, Tabora.
Katika mahubiri yake Askofu Mkuu Ruzoka amesema ili
padri afanikiwe katika utume wake hana budi kujitegemeza kwa Kristo mwenyewe na
kuwa tayari kutumia karama zake kwa faida ya wote.
Akirejea maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo, (Lk
10:1-9 ), Askofu Mkuu amesema hata Bwana wetu Yesu kristo aliwatuma wawili
wawili baada ya kuwafunda na wao kuwa tayari kujitegemeza kwake .
Ndani ya Misa hiyo Takatifu , Daraja ya Upadri
ilitolewa kwa Shemasi Ignas Gerald Akilimali wa Parokia ya Mt. Teresia wa Mtoto Yesu. Akimuasa Shemesi huyo amesema
padri ni mhudumu wa Hekalu la Bwana hivyo anapaswa kujitoa mzima kwa ajili ya
Kristo na Kanisa lake.
“Padri katika utume wake hana budi kuishi roho ya
upendo, na kwa kufanya hivyo anawafanya watu walio chini yake wampende Mwenyezi
Mungu.” Amesema.
Pia Askofu Mkuu Ruzoka amewaasa mapadri wote
kutekeleza utume wao kwa upendo, unyenyekevu na moyo wa shukrani.
“Mapadri waige mfano wa mwito wa Kristo kuwa na
busara wanapotekeleza majukumu yao kwani yapo maeneo watapokelewa na mazingira,
mengine watakataliwa hivyo wasikate tamaa.”
Aidha Askofu Mkuu amebainisha kuwa shabaha kuu ya
padri iwe ni kuwafikisha watu mbinguni na si vinginevyo.
Askofu Mkuu amewashukuru wazazi wa padri na wote
ambao watoto wao ni mapadri na watawa kwa kumpa Mungu zawadi ya thamani. Pia amewaomba wakristo wote kuendelea kuombea
miito mitakatifu ya upadri na utawa ili Kanisa lisipungukiwe wahudumu.
Waamini wamemuunga mkono Askofu Mkuu Ruzoka kwa
kumzawadia padri Ignas Akilimali gari dogo aina ya Rav 4 lenye thamani ya
shilingi milioni 12 na nusu pesa za kitanzania.
Comments
Post a Comment