“Mapadri msisahau wajibu wenu”






n Na Emanuel Mayunga, Sumbawanga

ASkofu wa Jimbo Katoliki Sumbawanga Mhashamu Damian Kyaruzi amewataka mapadri nchini kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia waamini na zaidi kumhubiri Kristo kwa sakramenti yaani kitubio, ekaristi takatifu, kipaimara, ndoa na mpako wa wagonjwa kadiri ya liturujia ya Kanisa Katoliki, mafundisho na mapokeo yake.
Askofu Kyaruzi ameyasema hayo katika homilia wakati wa maadhimisho ya misa ya upadrisho wa padri Boniphace Sichalwe na padri Leonard Halinga iliyofanyika parokiani Tunduma jimboni Sumbawanga.
Askofu amesema kuwa padri ni mtu wa imani na mkereketwa wa imani anayeitwa katika wito ili kuimarisha watu. Akaongeza kuwa ni jukumu la padri kuwajibika kueneza imani kwa niaba ya jumuiya na si kwa niaba yake yeye mwenyewe.
“Fumbo la Kanisa  au Mwanga wa mataifa   hati ya mtaguso wa pili wa Vatikani namba tisa, linasema  ilimpendeza  kuwatakatifuza na kuwaokoa watu siyo mmoja mmoja na pasipo muungano kati yao, bali kwa kuwaunda kama Taifa moja  lenye kumjua katika ukweli na kumtumikia kitakatifu.
“Kwa neema ya Mungu mmejaaliwa ukuhani wa bwana, mapadri ni wajibu wenu kutekeleza wajibu wa kugawa mafumbo matakatifu mkiwa wakereketwa wa imani, mtake na mtamani na watu wengine wawe kama ninyi mnavyoamini. Hubirini kwa ufasaha kwa wasiomjua Mungu waweze kumuongokea na wanaomjua waimarike zaidi na zaidi katika imani yao na wamtukuze Mungu,” amesema Askofu Kyaruzi na kuongeza kuwa;
“Kwa njia ya Nabii Yeremia  sura ya 1:10 inasema kuwa,  angalia  nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme ili kung’oa na kubomoa na kuharibu na kuangamiza ili kujenga na kupanda, kafanyeni kazi ya kuhubiri neno la Kristo ili kuwasaidia waamini kupokea huduma za sakramenti mbalimbali.
Kama Yesu alikua ni ndiyo basi hakikisheni mnawatumikia watu kadiri ya utume wenu wakati wote. Watumikieni wote sababu wana imani nanyi wakitegemea huduma zenu pasipo kinyongo na mtambue kuwa mmewekwa kwa ajili ya watu si kwa ajili yenu.
Ndiyo ya Yesu ndiyo ya padri, ni kauli mbiu katika mwaka wa mapadri  na iwaongoze katika kutenda na kunena mkifuata ndiyo ya Mungu kupitia nafsi ya mwanae bwana wetu Yesu Kristo.”
Wakitoa shukrani zao za dhati mapadri hao wameahidi kufanya kazi kwa uaminifu mkubwa wakiwa kama mapadri vijana wanatambua umuhimu wa kutumia vyema nguvu za ujana na kuomba ushirikiano kwa waamini na makreli wenzao pamoja na watawa.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya upadri aliyotujalia, na zaidi tunamuomba atuongoze na azidi kutembea nasi katika utume na wito wetu kama inavyostahili kwa watumishi wa Mungu. Tunamshukuru Mhashamu Baba Askofu kwa kutulea mpaka kufikia hapa tulipo na zaidi kwa kukubali kutupatia daraja takatifu ya upadri, shukrani kwa baba Mkurugenzi wa miito Jimbo padri Didas Nandi, paroko wa Parokia ya Tunduma na mapadri wote, watawa, waamini na zaidi kamati ya upadri na wote walioshiriki katika kufikia daraja ya upadri,” Amesema padri Leonard Halinga.
“Tumetwaliwa kutoka kwa watu ili tuwatumikie watu, tunawashukuru wazazi kwa kutuleta duniani na kututoa kwa Kanisa ili tutumike. Tukiwa kama mapadri vijana ni wajibu wetu kutumia nguvu za ujana wetu kwa ajili yenu na kwa ajili ya Kanisa na tunaomba mtuombee na sisi tunaahidi kuwaombea na kuwatumikia,”  Amesema padri Boniphace Sichalwe.
Akikabidhi zawadi kwa niaba ya Kamati ya upadrisho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Daudi Okechi amewashukuru waamini wa parokia ya Tunduma, Jimbo Katoliki Sumbawanga na wana kamati wote kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kufanikisha shughuli hiyo ambapo jumla ya kiasi cha shilingi 60,500,000 ziliweza kuchangwa ambapo milioni 43 zimetumika kununua magari mawili aina ya Toyota Hillax Surf ikiwa ni zawadi kwa ajili ya mapadri na kiasi kingine kutumika kwa ajili ya kufanikisha shughuli hilo.
Padri Boniphace Sichalwe na padri Leonard Halinga ni zawadi pekee ya mapadri jimboni Sumbawanga waliojongea daraja takatifu kwa mwaka huu wa 2017 ambapo Kanisa la Tanzania linafanya Jubilei ya Miaka 100 ya Upadri  na wote wanatokea parokia ya Familia Takatifu Tunduma na kuitwa mapacha katika upadri kwa kuzaliwa parokia moja na kupadrishwa mwaka mmoja, siku moja na Askofu mmoja ambapo jumla ya wanakamati 241 walishiriki kikamilifu katika kufanikisha kujongea utume wao, kamati hiyo ikiongozwa na Daudi Okechi akisaidiwa na Laurance Kyando, Thomas Almasi, Ester Njau na Genies Oisso.

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI