‘Mimba Shule za Kanisa marufuku” Ask Dallu
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea
Mhashamu Damian Dallu amesema kuwa anaunga mkono hatua ya Rais John Magufuli
kutoruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo, na kusema kuwa
shule zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki hazitaruhusu wanafunzi wanaopata
ujauzito kuendelea na masomo.
Amesema hayo katika Ibada ya Misa
Takatifu ya Upadrisho wa Shemasi Jerome Mtatifikolo, iliyofanyika katika
Parokia ya Bikira Maria Afya ya wagonjwa Ilole jimboni Iringa ambapo
amebainisha kuwa wanaoshabikia wanaopata mimba kurudi shule wanaharibu
utamaduni wa kiafrika na kuchafua heshima ya Taifa.
“Hayo mambo siyo sehemu ya utamaduni
wetu wa Afrika, ni mambo ya kigeni yanayotaka kutuchafulia utamaduni wetu.
Nawashangaa eti wanapigania haki ya tendo la ndoa, haki ya wapi hiyo?. Tutakuwa
na shule za namna gani zinazoruhusu mwanafunzi kwenda kulea mtoto kisha arudi
tena na akipata mimba nyingine aende tena nyumbani?” Amehoji Askofu Dallu.
Katika hatua nyingine Askofu Dallu
amewaasa waamini kufanya maandalizi ya kutosha hasa ya kiroho wanapojiandaa
kuingia katika Sakramenti ya Ndoa ili ndoa zao ziwe na mwelekeo wa kiimani
zaidi. Amesema kuwa kabla ya kupewa upadri, Shemasi Jerome alihudhuria mafungo
ya kiroho ya siku 5 jambo ambalo linapaswa kuigwa na wale wanaojiandaa kupokea
Sakramenti ya ndoa badala ya kujikita katika kufanya maandalizi ya kimwili.
“Watu wa familia mnatumia siku ngapi
kufanya mafungo kabla ya kufunga ndoa? Au ndiyo ile kufanya maandalizi mengine
ya kimwili marefu. Mkumbuke kuwa hata sisi mapadri tunatoka kwenu, matokeo ya
kukosa maandalizi ya kutosha kabla ya ndoa ndiyo haya tunayoshuhudia sasa hivi
ambapo wanaoishi ndoa kama Sakramenti ni wachache,” ameeleza.
Aidha amesema kuwa watu wanaoishi
maisha ya pamoja kwa muda mrefu hadi kuwa na watoto hawastahili kuitwa wachumba
kwa kuwa uchumba kielelezo chake ni Maria na Yosefu, na kuwataka kuacha kutumia
jina hilo na badala yake wajiite wachumba sugu.
“Ulisikia wapi watu wanaishi uchumba
mpaka wanakuwa na wajukuu? Tafuteni jina jingine kuanzia sasa labda mjiite
wachumba sugu. Tutapata mapadri na masista wa namna gani? Kielelezo cha uchumba
ni Yesu na Maria,” Ameeleza.
Pia amesema kuwa kazi ya karama ni
kujenga umoja wa Kanisa na siyo kuligawa, na kumtaka kila mmoja kutumia wito
wake kumtajirisha mwingine.
Hapo nakuunga mkono Baba Askofu.Mungu akutie nguvu!
ReplyDeleteHalafu mtutawale vizuri siku yenu yaja
ReplyDelete