Viongozi wa Dini nchini
wameshauriwa kutazama kwa kina mafundisho wanayoyatoa kwa waamini wao, hasa kwa
wakati huu ambao dunia imemezwa na Utandawazi, kwa kuyaelekeza zaidi katika kuamsha ari mpya
ya kuokoa kizazi kijacho ambacho ni vijana na watoto, ambao wengi wao pia
wamemezwa na mmomonyoko wa maadili.
Wito huo umetolewa
hivi karibuni na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mizengo
Pinda, wakati akiongoza maadhimisho ya Miaka 21 ya Uinjilishaji wa Redio Maria
hapa nchini Tanzania, yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Kanisa Kuu la
Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki Mbeya.
Waziri Mkuu Mstaafu Pinda
akiongelea suala zima la mmomonyoko wa maadili ambalo linaonekana kuwameza
vijana wengi, amesema hali iliyopo sasa si alama nzuri kwa Kanisa la kesho,
ambalo linategemea miito mitakatifu kutoka kwa kizazi hiki cha sasa, ambacho
kinaonekana kumezwa zaidi na malimwengu na kujiweka nyuma katika masuala ya
Imani.
Akitolea mfano
ushiriki wa Jumuiya ndogondogo, amesema kuwa vijana wengi na watoto hawahudhurii
huko, ikiwemo pia ushiriki wao kwa mambo ya Kanisa ni wakusuasua, huku akitolea
mfano kwenye familia yake ambayo anaishi na vijana wengi, “Mfano pale nyumbani
kwangu na Mama Pinda tunalea vijana wengi mno lakini katika suala la kusali na
kwenda Jumuiya ni wazito sana, ikitokea tunawalazimisha kusali pamoja usiku
sala wanazo sali nyingi hazina tafakari (meditation) na mara nyingi zinakuwa za
harakaharaka, hali ambayo ni tofauti na unapowakuta wakiwa wanatizama luninga,
kucheza game,au namna wanavyutumia muda mwingi katika simu zao za mkononi,” Amesema
Pinda.
Aidha, amezikumbusha
familia za kikristo kila moja kurejesha ule utamaduni wa zamani wa kusali
pamoja usiku hasa sala ya Rozari Takatifu, sambamba na kuwafundisha watoto na
vijana kusali kwa kutafakari, huku akizitaka familia kutokujisahau kwa kumezwa
na majukumu na kusahau suala la malezi kwa familia zao, ikiwa ni pamoja na
kuzungumza na kula pamoja nao hasa siku za mwisho wa juma na zaidi jumapili na
siku nyingine za mapumziko.
Kwa upande wa redio
Maria Tanzania, Waziri Mkuu Mstaafu ameishauri redio hiyo kuhakikisha kwamba
inaandaa vipindi vyenye kuelimisha jamii kiimani, hasa kutoa mafunzo
yanayoelekeza kuondokana na imani za kishirikina ambazo bado zipo katika jamii
ya watanzania wa leo, ambapo akatolea mfano mauaji ya Albino,”Padri Maendeleo
na timu yako nawashauri mjikite pia katika kutoa mafundisho yanayoelekeza watu
kuondokana na dhana ya ushirikina, na badala yake muwaelekeze katika kufanya
kazi kwa bidii na kuishi kwa kumtegemea Mungu zaidi,” amesema Pinda.
Aidha hakusita
kuwasisitiza waandaaji wa vipindi kwenye redio za Kanisa kujitika zaidi katika
kuandaa vipindi vingi vinavyojenga maadili kwa vijana, kwa lengo la kuimarisha
miito na kujenga taifa lenye watu wanaofuata maadili hata katika kuwatumikia
wanajamii, na vitakavyowajengea uaminifu katika imani yao hivyo wataondokana na
dhana mbovu iliyopo kwa wakati huu ya waamini kuhama makanisa kila kukicha kwa
lengo la kutafuta miujiza na vitakavyowafanya walipende Kanisa na wajisikie
fahari kulitumikia.
Wakati huo huo,
Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evarist Markusi Chengula I.M.C, aliyeongoza
ibada ya misa Takatifu ya kilele cha maadhimisho ya miaka 21 ya redio Maria Tanzania, amewashukuru viongozi
wa redio hiyo akiwemo Rais Julius Kira na Mkurugenzi Padri John Maendeleo CSSp,
kwa kupeleka maadhimisho hayo jimboni kwake, ambayo yamemfanya aweze kukaa meza
moja na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya mkoa ambao hajawahi kukutana nao
na kuzungumza nao kwa kipindi chote cha uongozi wake kama Askofu wa Jimbo hilo.
Kilele cha
Maadhimisho ya Miaka 21 ya Uinjilishaji wa redio Maria Tanzania tangu
kuanzishwa kwake, kilifanyika Julai 2 mwaka huu, ambapo katika maadhimisho hayo
aliyekuwa mgeni rasmi Mh Pinda aliongoza harambee ya kuiwezesha redio hiyo na
zilipatikana jumla ya shilingi milioni 25, ahadi zikiwa ni shilingi 13,128,000
na pesa taslimu zikiwa ni shilingi 11,872,000.
Hata hivyo maadhimisho
hayo yalitanguliwa na Hija ya kiroho ya siku 5 kwa mahujaji waliotoka katika
majimbo Makuu ya Songea, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, pamoja na majimbo ya
Zanzibar, Singida, Moshi, Iringa, Mpanda, Mtwara, Ifakara, Mbinga wakiwemo
wenyeji Jimbo Katoliki Mbeya, walitembelea katika maeneo mbalimbali likiwemo
Kanisa la Hija Mwanjelwa, kupanda mlima wa Hija Loleza, kutembelea daraja la
Mungu na kushiriki mafundisho ya kiroho toka kwa mapadri mbalimbali wa Jimbo
Katoliki Mbeya akiwemo Padri Anthon Makunde aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania miaka ya nyuma.
|
Comments
Post a Comment