Papa Francisko: Siku ya Kimataifa Ya Mzee Nelson Mandela

Baba Mtakatifu Frsancisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuvuka mifumo yote ya ubaguzi, hali zote za kutovumiliana pamoja na udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu! Baba Mtakatifu anaandika ujumbe huu wakati Umoja wa Mataifa unapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2009 na kuanza kuadhimishwa rasmi tarehe 18 Julai 2010 kama njia ya kumuenzi Mzee Nelson Mandela aliyejisadaka kwa ajili ya kupigania uhuru, haki msingi za binadamu na demokrasia ya kweli inayowaambata wananchi wote wa Afrika ya Kusini. Ni kiongozi aliyesimama kidete, kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, vitendo vilidhalilisha utu na heshima ya binadamu!

Mzee Mandela aliwahi kusema, ni rahisi sana kuweza kuvunjilia mbali mifumo ya kibaguzi, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, jamii inaunda mashujaa watakaojifunga kibwebwe usiku na mchana ili kulinda, kutetea na kudumisha haki na amani duniani.  Leo hii dunia imegawanyika na kusambaratika sana kutokana na sababu mbali mbali, inahitaji mashuhuda na wajumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu, watakaoweza kusimama kidete kupambana na changamoto zinazowakabili vijana wa kizazi kipya; ukosefu wa haki, amani na maridhiano kati ya watu sanjari na kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kwa kutekeleza yote haya, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa kweli inaendelea kumuezi Mzee Nelson Mandela.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI