Muigizaji maarufu mateso ya Yesu Kristo asaka mrithi wake

MUIGIZAJI maarufu  wa mateso  ya Yesu Kristo  katika msalaba hasa katika kipindi cha Kwaresima   ameelezea  Hija  ya wana utume wa Fatima ya jimboni Mbeya iliyofanyika kijimbo katika Parokia ya Izuo umbali ya kilomita 24 kutoka katika Kigango cha Izuo hadi parokiani hatoweza kuisahau kutokana na kipigo cha ukweli alichopata kutoka kwa  askari wa kiyahudi sanjari na kupoteza fahamu.
George Patson Mtambo  amesema  tangu ameanza kuigiza  kama Yesu Kristo  kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita baada ya kurithishwa na marehemu padri Mpepo katika Parokia ya Mwambani  na kuendelea, amesema kupitia njia yake ya msalaba  aliyoifanya  Izuo hawezi kufananisha aliyowahi kufanya Ileje katika Parokia  ya Itumba, Mwambani na katika Mlima Loleza hajawahi kukumbwa na hali kama iliyomtokea katika Hija hiyo.
Akizungumza  na KIONGOZI   mara baada ya ibada ya misa takatifu ya  Jumapili ya hitimisho la Hija hiyo, Mtambo amemuomba Mwenyezi Mungu  kupitia Hija hiyo  aweze kumsamehe madhambi yote aliyowahi kuyatenda  na kwamba iwe  kama sehemu ya malipizi yake ili aje kuonja ufalme wa mbinguni.
“Kwa haki sintoweza kuisahau njia ya msalaba katika  Hija hii…kwani nilipigwa kibao cha ukweli  na  kuna kipindi nilianguka  siyo kwa kuigiza  lakini ni kweli nilielemewa na kuishiwa nguvu na kadiri nilivyozidi kuelekea kituo kimoja kwenda kingine nilizidi kuelemewa  na msalaba ambao ulikuwa ni mzito sana  na safari ya milima na mabonde  ilikuwa ndefu  sana,’anasimulia
Ameendelea kusimulia siri nzito ya yaliyomkuta kuwa,” ninakumbuka ghafla  nilipigwa na usingizi mzito ulipowadia muda wa kuigiza sasa ninakata roho pale nilipotamka,”Baba  wasamehe kwani hawajui watendalo……Mungu wangu!!Mungu wangu mbona umeniacha,”na nilipotamka kuwa,” imekwisha roho yangu naiweka mikononi mwako,” sikuweza kumalizia  na ndipo nilipoteza fahamu.
Ameelezea  igizo lake la Hija iliyofanyika katika parokia ya Izuo kwamba kwa kipindi chote  alichowahi kuigiza  hakuwahi kupoteza fahamu lakini pia kipigo alichokipata ikiwemo na msalaba mzito uliomuelemea na safari ndefu ya umbali wa zaidi ya kilomita 24 kutoka kigango cha  Isuto hadi parokiani Izuo.
 Amezungumzia  alivyotandikwa kibao  katika kituo cha tatu na kuchapwa na mijeredi hadi akaanguka kwa ukweli huku akielezea alivyoshikwa na butwaa kuwa watu ambao ni wazee na heshima zao  na wananchi wengine wa dini nyingine  wakiwa wamesimama, wakivua kofia kwa heshima, wakiinama kwa ishara ya kuheshimu huku magari na pikipiki zikiegeshwa  pembeni kuipisha  safari hiyo.
Ameelezea  tukio jingine  la ajabu   ambalo hakuwahi kuliona tangu  ameanza kuigiza ni  baadhi ya  wananchi  kuzoa  mchanga katika ile  alama ya mfano wa damu  zilipokuwa zikimwagika na alipoanguka na kufunga  katika nguo zao.
Hata hivyo ameelezea kile kitendo cha  kuvuliwa nguo  na hakika alikumbwa na hisia kali na alishindwa kujizuia na alianza kulia  na baadaye  anakumbuka hadi kule makaburini alipobebwa na  jeneza  halisi linalotumika kubebea  miili ya  marehemu kwenda kuwazika.
George  amesema  kuwa ameweka mikakati  kuhusu njia ya msalaba kuwa atarithisha   mapema   ambapo katika Hija ya kitaifa ya mwezi Oktoba,2017  itakayofanyika  kupandisha Mlima Loleza  atakuwa naye jirani  na kwamba hana mpango wa kustaafu  kwa sababu  kwake anaona ni kama wito lakini  ni vyema ukafikia muda   Mungu akimjalia kufikia umri  wa  uzee  na nguvu zitakapopunguwa  za  kuigiza awe tayari ameshamwachia mrithi wake   kwa sababu  katika mateso  ya Yesu hakuonekana  hadi uzee wake.
“Vijana wakubali kupokea maisha ya kiroho, hakuna kilicho kigumu mbele ya Mwenyezi Mungu na Mungu atatenda maajabu yake,” na ameelezea kuwa ameanza  kuigiza tangu akiwa bado mtoto mdogo   mwaka 1972 katika Parokia ya Mtakatifu Maurus Kurasini alikuwa akiigiza siku za  sikukuu ya Pasaka na Noeli.
 Na anakumbuka walipoandaa  onesho la njia ya msalaba mateso ya Yesu Kristo  wakiwa  na mzungu mmoja aliyemtaja kwa jina la Jemong, wakishiriki maigizo  na  Mkuu wa Mkoa wa sasa wa Dodoma Jordan Rugimbana kwa ushirikiano  na Askofu  wa KKKT, Alex Malasusa  kwani walikuwa wakishirikiana  kuandaa na kufanya maigizo kwa pamoja  wakati huo.











n Na Thompson Mpanji, Mbeya


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI