KUELEKEA MIAKA 100 YA UPADRI: KILOMBERO WAPATA PADRI WA KWANZA MJESUITI
Na Tuzo Nyoni, Ifakara
Wakati maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya
Upadri nchini yatakayofanyika katika Jimbo Kuu Katoliki Dodoma yakiendelea
vizuri, wito kwa mapadri nchini umeendelea kutolewa kuwa wazingatie kuwa
wametumwa kwa watu ili wawasaidie kuondokana na matatizo mbalimbali na hatimaye
wajisikie kuwa wao pia ni wana wa Mungu.
Akihubiri katika adhimisho la misa takatifu ya shukrani ya
Padri Patrick Ngamesha(PICHANI) iliyofanyika hivi karibuni katika Kanisa la Mtakatifu
Siliakus parokiani Mang’ula Jimbo
Katoliki Ifakara, Padri Valelian Shirima aliyewahi kuwa Mkuu wa Shirika la
Majesuiti amesema kuwa Kanisa lote la
Mungu lina haki ya kusherehekea sikukuu
hiyo kwa ajili ya makuu aliyoyatenda kupitia nafsi ya padri mpya Patrick
Ngamesha.
Padri Shirima amesema mapadri wamepewa mamlaka ya
kuwasafisha watu dhambi zao na wanapokutana na watu wenye mioyo migumu
wasichoke kuwahubiria neno la Mungu, kazi ambayo mapadri wanaifanya katika
maisha yao yote na wakumbuke kwa sababu yao watu wengi watakuja kumwabudu na
kumshuhudia Kristo, na tuzo lao
halitakuwa dogo.
Aidha Padri Shirima amemtaka Padri Patrick Ngamesha ambaye
ni mjesuiti wa kwanza wa bonde la mto Kilombero (majimbo Katoliki Ifakara na
Mahenge) kuwa mtu wa sala na kabla ya
kufanya kitu chochote akumbuke kuanza kwa sala ili kazi yake iwe ya kumpendeza
Mungu na aweze kuunganika naye.
“Mapadri wanatakiwa wakumbuke kuwa Mungu hakuwaita kuja
kulipiza kisasi na kuwatakia mabaya watu wabaya, bali wameitwa ili wawatakatifuze
watu na kuwatia moyo ili wawe watu wanaomfuata Kristo,” Amesema Padri Shirima.
Hata hivyo amewakumbusha mapadri kuwa tayari kutumwa popote
kufanya utume, tegemeo lao likiwa Kristo mwenyewe atakayewawezesha katika utume
wao huku wakiepuka kuwa kikwazo kwa kila watakayekutana naye.
Padri Ngamesha alipewa Daraja takatifu ya Upadri tarehe 7
Julai mwaka 2017 katika parokia ya Msimbazi Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam na
Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo Mhashamu Eusebius Nzigilwa.
Comments
Post a Comment