Serikali yasisitiza Bunge kutooneshwa mubashara

n Na Damasus Mtalaze, Kibakwe

SERIKALI  imeendelea  kusisitiza  kuwa azma yake ya kutokuonesha  Bunge  moja  kwa   moja kuwa ni kutokana na matumizi ya lugha  zisizofaa  za  matusi  na  badala yake itaendelea  kuonesha  vipindi  vya  Bunge  sehemu  ya  maswali  na  majibu  kwani  eneo  hilo linawafaa  watanzania  wote  kwa  sababu  wanapata  majibu  ya moja  kwa  moja  ya  Serikali  kwa  matatizo  yanayowakabili .   
Hayo  yamesemwa  na  Waziri  Ofisi  ya  Rais  Tawala  za  Mikoa    na  Serikali  za  Mitaa-TAMISEMI Mhe.  George Simbachawene  katika  mkutano  wa  hadhara  uliofanyika  katika  kijiji  cha  Pwaga  wilayani  Mpwapwa  hivi  karibuni.
Waziri Simbachawene  amesema  kuwa  baada  ya  Serikali  kuona  lugha  zisizofaa  zikitolewa  bungeni, imeona  si  vyema  kuonesha  Bunge  moja  kwa  moja  kwa  sababu  lugha  nyingi   zisizofaa   haziwafai   watanzania kwani hazifundishi  zaidi ya kupotosha na  kuharibu  maadili  mema  yaliyojengeka  katika  jamii   na  hasa  kwa   watoto.
Mhe. Simbachawene  amesema  kuwa  Serikali  imeona  ni  vyema  kuzuia Bunge zima kuoneshwa    na  badala  yake  kuoneshwa  vipande  vya  maswali  na  majibu  kwa  sababu  hakuna  lugha  zisizofaa  zinazotolewa sehemu  hiyo  na  kuwa   sehemu  hiyo  Serikali  inapata  nafasi  ya  kuwajulisha  watanzania   kuhusu  utatuzi  wa  shida  zao   kutokana  na  swali  la  Mbunge  mhusika   aliyetaka  kujulishwa  tatizo  la  wananchi  wake .
“Watanzania  wenzangu   mtu  anasimama   anamtukana  Mbunge  mwenzake,  mnataka   Serikali  ioneshe, Mbunge  anamtukana  waziri  Serikali  ioneshe, Mbunge  anamtukana   Rais, sisi  wabunge  tutakuwa  tunawafundisha  nini  watoto   wetu? watoto  wakikosa  maadili  mema  nani  wa  kulaumiwa  kama  siyo  sisi  wabunge  tunaotunga  sheria?” amehoji Waziri Simbachawene.
Amesema  watanzania  wana  shida  zinazohitaji  utatuzi  na  si  lugha  chafu  au  matusi. Ameongeza kuwa   siku  zote  maneno  yasiyofaa  hayaifai  nchi  na  badala  yake  yanabomoa  na  kuwatoa  watanzania  kwenye  umoja, mshikamano, upendo na  udugu  wao . Amesema  utawala  wa  awamu  ya  tano  hautakubali  tunu hizo  zipotee  kwa kufumba  macho  kama  vile  Serikali  haioni  madhara  yake,  kwani  lugha  za  matusi  si  maadili  ya  watanzania.
Kuhusu tatizo la  maji  kwa  kijiji  cha  Pwaga, amemwagiza Mkurugenzi  wa  wilaya  hiyo  Bwana Mohamed  Maje kuwa  wale  wote  walio katika vyanzo  vya  maji  wawe  wamehamishwa  ndani  ya  siku  14 na  kuwa  taarifa  hiyo  iwasilishwe  ofisini  kwake  haraka. Amesema  ni  vyema  kupata  ufumbuzi  huo  mapema ili  watu wasiendelee  kuteseka  wakati  waharibifu  wapo  wanaonekana.
“Maeneo  ya  vyanzo  vya  maji  yasipotunzwa  watanzania watateseka, kwa  hiyo  ni  vyema  kujihadhari  mapema  kabla maisha  ya watanzania  hayajafikia pabaya.” amesisitiza   Mheshimiwa  Simbachawene .      


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI