Mashemasi na Mafrateri waonywa kuepuka ubinafsi
ASKOFU wa
Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evarist Chengula (IMC) amewaalika mashemasi na
mafrateri kuacha ubinafsi na badala yake
waendelee kudumisha umoja, mshikamano na upendo kama wanavyoishi sasa huku akionesha matamanio yake ya kupata
mashemasi na mafrateri watanzania wenye
asili ya Asia.
Akizungumza
katika kikao cha mwaka cha mashemasi na
mafrateri kilichofanyika katika Ukumbi wa Parokia ya Mbeya Mjini, Askofu
Chengula amewapongeza kwa kuishi kama ndugu wamoja na wazaliwa wa Jimbo Katoliki Mbeya licha ya kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Katika
kikao hicho cha mwaka mashemasi na
mafrateri kutoka nchi mbalimbali ikiwemo
Nigeria, Benin na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pia nje ya Jimbo
Katoliki Mbeya, Tanzania Bara na visiwani wamekuwa wakikutana na Askofu kuzungumzia masuala ya kimwili na kiroho.
“Ninawapongeza mnavyoishi… kama wote ni wazaliwa wa Mbeya na muendelee kuwa na umoja, upendo na
mshikamano huo huo kwani ninyi ni familia moja ya Yesu Kristo huku mkiendelea
kumtanguliza Mungu ili wote muweze kupitia
madaraja yote matakatifu kadiri Mwenyezi Mungu atakavyopenda,”amesisitiza.
Aidha
Askofu Chengula ameonesha matamanio yake
ya kupata mafrateri, mashemasi na hata mapadri raia wa Tanzania
wenye asili ya Asia kutoka katika Jimbo lake, ”nimekuwa nikitamani
sana kupata mafrateri na mashemasi
wahindi na wazungu lakini wawe wa Jimbo letu.”
Askofu
Chengula amewaalika kujiweka tayari kwenda kufanya kazi za kichungaji katika
majimbo mengine nje ya Jimbo Mbeya na
popote duniani kama walivyo mapadri wa
Jimbo ambao wanafanya kazi za kichungaji nje ya Jimbo.
“Muwe na moyo wa utayari wa kwenda kufanya
kazi katika majimbo mengine kama kaka
zenu(mapadri) kadiri ya uhitaji huku mkiondoa umimi mkiongozwa na Sala kuwa
ndiyo mafuta ya safari yetu,” amesisitiza.
Comments
Post a Comment