Wanawake waomba Sheria ya Ardhi itafsiriwe kwa kiswahili
WANAWAKE nchini wameiomba Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutafsiri sheria mbalimbali ikiwemo ya ardhi
kwa lugha ya Kiswahili na kutoa elimu hiyo ili kuwasaidia wanawake wa vijijini ambao wamekuwa wakikosa
haki zao kwa kutokujua sheria hizo.
Hatua hii imekuja baada ya wanawake
wengi kulalamika kudhulumiwa ardhi na baadhi ya viongozi wa vijiji huku
wakiachwa bila malipo hali inayowadidimiza kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na
Afisa habari wa Jukwaa la wakulima wanawake wa Tanzania Melea Sulutya wakati
akisoma risala katika Kongamano la wanawake lilioandaliwa na Shirika lisilokuwa
la kiserikali linalosaidia vikundi vya wakulima (Action Aid) katika Kijiji cha
Mloda Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.
Sulutya amesema kutokuzielewa sheria
zinazomlinda mwanamke hasa katika masuala ya kumiliki ardhi kumefanya wanawake
wengi kuendelea kuishi katika manyanyaso bia kujua jinsi ya kudai haki zao.
Wakati huo huo mwanamke mmoja (jina
linahifadhiwa) mkazi wa kijiji cha Buigiri amesema wanawake wanadharauliwa
kiasi kinachowafanya kukutana na ugumu wa maisha huku akitumia nafasi hiyo
kuomba msaada wa sheria juu ya kesi yake ya kubakwa ambayo mtuhumiwa alipewa
hukumu ya kulipa faini ya shilingi laki tatu ambayo haiendani na kosa
alilofanya.
“Nilibakwa na mwanaume ambaye mpaka
sasa naishi naye kijiji kimoja, kitu hiki kinaniumiza sana..mtu amebaka halafu
anatozwa faini ya shilingi laki tatu!moyo wangu unaniuma sana kwa kuwa najua
hali hii ikiendelea hivi wanawake wengi watazidi kubakwa,”amesema mwanamke
huyo.
Naye Mratibu uwezeshaji umma kifedha
katika sekta ya kilimo (Action Aid)
Joram Wimmo amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025
asilimia 30 ya wanawake wawe wanamiliki ardhi na kuzalisha katika ardhi hizo.
Kwa upande wake mwakilishi wa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Elias Wilson amesema kuwa ni
jukumu la Halmashauri kuhakikisha vikundi vinavyoanzishwa na wahisani
vinaendelezwa na kuwasaidia wananchi wengi zaidi.
Comments
Post a Comment