UPATANISHO: KARATU WAANDAA MISA MAALUM
Na Sophia Fundi, Karatu.
PAROKIA ya Karatu katika
Jimbo Katoliki Mbulu kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe mwaka 1946 imeadhimisha
misa ya upatanisho kwa walei na mapadri waliowahi kufanya utume katika parokia
hiyo akiwemo marehemu padri John Costigan wa Shirika la wapalotini ambaye ndiye
mwanzilishi wa parokia hiyo.
Misa hiyo ni hitimisho
la Mfungo wa Novena ya siku tisa ya kuomba Huruma ya Mungu ambapo waamini
walishiriki katika Jumuiya ndogondogo za kikristo na hatimaye kushiriki adhimisho
la misa iliyohudhuriwa na mapadri zaidi ya 30, wakiwemo mapadri wote waliowahi
kufanya utume katika parokia hiyo na mwakilishi wa Shirika la wapalotini ambaye
ni mkuu wa Shirika hilo jimboni Mbulu, viongozi wa Serikali katika Wilaya ya
Karatu, wabunge Jimbo la Karatu, viongozi wa siasa na wazee maarufu.
Akihubiri katika Misa
hiyo, paroko wa parokia hiyo padri Pamphili Nada amesema kuwa tukio hilo la
kuadhimisha misa ya upatanisho ni zoezi lililoibuliwa na walei wa parokia hiyo kupitia
umoja wa wazee na mapadri waliowahi kufanya utume katika parokia hiyo ambapo
waliamua kufanya adhimisho la misa katika adimisho la somo wa Kibawata parokia
ya Karatu ya Mtakatifu Yakobo mtume Julai 25 ya kila mwaka.
Akizungumza kwa niaba ya
wawakilishi wa walei, Mwenyekiti wa parokia Bw. Reginard Bayyo amesema kuwa
parokia imeamua kufanya adhimisho la misa takatifu ya upatanisho kwa lengo la
kuwaomba msamaha mapadri waliowahi kufanya utume katika parokia hiyo
waliotangulia mbele ya haki na wanaofanya utume maeneo mbalimbali kwa yote
waliyowakosea hasa padri Costigan ambaye anadaiwa kuondoka bila amani katika
parokia hiyo na kurudi kwao Ireland miaka ya 1972 ambapo walei
wamelifikiria na kuona kuwa hakufanyiwa vizuri katika utume wake.
Katika adimisho hilo Mwenyekiti
huyo ameomba msamaha kwa niaba ya walei parokia ya Karatu kwa kumpa majani kama
ishara ya kuomba msamaha mwakilishi wa shirika la wapalotini padri John
Onna na pia kama ishara ya kuomba msamaha kwa niaba ya mapadri wote
waliowahi kufanya utume katika parokia ya Karatu majani hayo alipewa padri John
Qadwe.
Akielezea historia ya marehemu
padri Costigan, Padri John Qadwe amesema kuwa marehemu alifanya kazi ya utume
katika parokia ya Karatu miaka ya 1949 hadi 1972 ambapo alihamishwa kwenda
kuanzisha parokia ya Endabash jimboni Mbulu lakini marehemu hakufurahishwa na
uhamisho huo na kuamua kujifungia chumbani kwake siku tatu bila kula chochote
na baada ya siku hizo aliondoka kwenda kwao bila kumuaga mtu yeyote.
Amesema kuwa kuondoka
kimyakimya kwa marehemu padri Costigan kuliwafanya walei parokia ya Karatu kuwa
na wasiwasi kwamba hakufurahishwa na kitendo hicho, ndipo walipoamua
kutafuta ndugu zake au mapadri wa Shirika lake kuwaomba msamaha kwa yote
yaliyotokea miaka hiyo kwa kuwashirikisha mapadri wote waliowahi kufanya utume
parokiani Karatu.
Mwakilishi wa Shirika la
wapalotini padri Onna baada ya kupokea majani ya upatanisho kutoka kwa Mwenyekiti
wa walei aliwashukuru kwa kutafuta upatanisho ambapo aliwaomba zoezi hilo liwe
endelevu katika familia na jumuiya ndogondogo za kikristo.
Comments
Post a Comment