MAWASILIANO YA JAMII YAUNGANISHE JAMII-PAPA FRANSISKO


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Furaha ya Injili anasema, daima wema huaka kusambaa. Kila mara ukweli halisi na wa uhakika unapotambulika, kwa asili yake unatafuta namna ya kukua ndani ya watu na mtu aliyewahi kuguswa na ukombozi huu anakuwa mwepesi kutambua mahitaji ya wengine. Kadiri unavyokua, wema unaota mizizi na kuendelea kukomaa. Waamini wakitaka kuishi maisha yenye hadhi bora, ili kuchuchumilia ukamilifu wake, kuna haja ya kutoka ili kuwaendea wengine na kutafuta mema yanayofumbatwa katika sakafu ya mioyo yao.
Hii inatokana na ukweli kwamba, upendo wa Kristo unawabidisha na kwamba, wanapaswa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa watu wa Mataifa. Mama Kanisa anawaalika waamini kujifunga kibwebwe tayari kuanza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama kielelezo cha imani tendaji! Mama Kanisa anatambua na kuthamini maendeleo ya sayansi na teknolojia katika sekta ya mawasiliano ya jamii kwani, yanatoa mchango mkubwa katika ukuzaji na ustawishaji wa nafsi za watu sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu!
Lakini, kuna haja pia ya kuwa waangalifu na matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kwani badala ya kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana, vimekuwa ni sababu ya kumong’nyoka kwa maadili na utu wema! Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza Padre Josè, maarufu kama “Bepe” Di Paola, ambaye hivi karibuni amefungua Kituo cha Radio kijulikanacho kama “Cristo de los Villeros” huko nchini Argentina. Anampongeza kwa kujisadaka ili kuhakikisha kwamba, wanatumia karama na vipaji mbali mbali walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kukuza na kudumisha mawasiliano, ili kujenga  umoja na mshikamano kati ya watu badala ya kuta za utengano.
Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kutumia karama zao kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu. Radio hii imezinduliwa kwa maneno ya Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kwa njia ya video uliotumwa kwa Padre “Bepe” Di Paola na kusikilizwa na waamini wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya uzinduzi wa kituo hiki cha Radio. Lengo ni kuweza kuwafikia watu wengi zaidi, hasa wale ambao wako pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu ambao wamebaki wakiwa wamehifadhiwa katika sakafu ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko.
Amewatakia heri na baraka waamini wa Parokia ya San Juan Bosco na vitongoji vyake bila kuwasahau wasaidizi wa karibu wa Padre Josè anapoanza utume huu mpya. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake, kwa kuwataka waamini wote kusonga mbele kwa imani na matumaini, kwa ari na moyo mkuu pasi na kukata tamaa. Padre Josè, maarufu kama “Bepe” Di Paola katika mahubiri yake amekazia umuhimu kwa waamini kujitambua kuwa ni Parokia, wanamopaswa kusaidiana kukua na kukomaa kiroho, kimwili na kiutu, tayari kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo. Amewataka waamini kufanya kazi kwa ari na moyo mkuu; kwa uvumilivu na subira! Watambue changamoto zilizoko mbele yao, yaani matumizi haramu ya dawa za kulevya, ghasia na vurugu; mambo yanayofumbatwa katika utamaduni wa kifo! Kama Parokia watapaswa kusimama kidete kulinda, kukuza na kudumisha Injili ya uhai, amani na upendo kati ya watu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI