‘Padri asiyependa waamini hakubaliki’ Ask Nzigilwa
IMEELEZWA
kuwa kitendo cha waamini kuwapenda mapadri wao ni matokeo ya namna ambavyo
mapadri wanajitoa kwa upendo katika kuwahudumia waamini hao. Hayo yamesemwa na
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa
katika Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu ya Upadri kwa shemasi Dominic
Mavula wa Shirika la Damu Azizi kutoka Parokia ya Mandela Jimbo Katoliki
Morogoro.
Askofu
Nzigilwa amesema kuwa padri anapaswa kutoa huduma yake huku akitambua kuwa
kupenda na kuwa na huruma ni nyenzo muhimu katika kuhusiana na kuhudumia
waamini. Amesema kuwa utume wa padri ni kuokoa roho za waamini na siyo roho
yake pekee.
“Sala,
moyo wa huruma na upendo ni sehemu ya utume wa padri. Mkiwapenda waamini nao
watawapenda kwa kuwa upendo ni lugha inayoeleweka na viumbe vyote. Hivyo
mjitahidi kuishi huruma na upendo wa kimungu, na kwa kufanya hivyo mtazipeleka
roho nyingi mbinguni” ameeleza.
Aidha
Askofu Nzigilwa ameongeza kuwa huruma ya padri kwa waamini ni lazima iendane na
roho na bidii ya kusali, kwa kuzingatia imani na usikivu katika sauti ya Mungu.
Hata hivyo Askofu Nzigilwa amewaasa waamini kuwapokea mapadri na kuwasaidia
katika mapungufu yao na kuwatia nguvu.
“Muwapokee
mapadri na muwasaidie, mfanye kazi yao iwe sababu ya wokovu kwao na kwenu. Wao
wameteuliwa kwa ajili ya utakatifu na kuokoa roho za waamini siyo kuokoa roho
zao pekee. Hivyo muwasaidie katika mapungufu yao na kuwatia nguvu” ameongeza.
Comments
Post a Comment