Wataalamu Wakristo wajiimarishe kiroho
CHama
cha Wataalamu Wakristo Tanzania (CPT) Jimbo Katoliki Kigoma kimewataka
wanachama wa utume huo kuishi maisha ya utakaso kiroho na kimwili ikiwemo
kujiimarisha kiuchumi katika kumtumikia Mungu.
Hayo ameyasema Katibu Mtendaji wa CPT
Jimbo Katoliki Kigoma (CPT) Fransis Mangu wakati akizungumza na Gazeti hili
katika kujua mipango mikakati waliyonayo ndani ya utume huo ambapo ametaja kuwa
wanapanga kujiimarisha kiroho sambamba na kiuchumi ndani ya Kanisa Katoliki.
Akitoa mfano kwa upande wa kiroho
amesema wamepanga kujiimarisha katika mambo ya imani kama kufanya Hija, mafungo
pamoja na sala na kwa upande wa kiutawala ni kueneza utume huu katika kujitanua
kiuchumi.
Hata hivyo Mangu amesema kuwa katika
Parokia 23 za Jimbo Katoliki Kigoma changamoto waliyonayo ni kwa upande wa
Parokia moja ya Kibombo ambapo wamejipanga kuwa ifikapo Septemba 30, watakuwa
na Hija katika Parokia hiyo itakayochukua siku mbili ili kuhamasisha utume huo
kuwaimara jimboni hasa upande wa kiroho na kimwili.
Aidha Katibu Mangu amesema kuwa wana
aina tatu za mikutano; timu ya Jimbo ambayo hukutana mara sita kwa mwaka,
pamoja na Halmashauri inayochukua viongozi watatu wa kila parokia na hukutana
mara mbili kwa mwaka katika kupanga mikakati juu ya kuendeleza malengo ya utume
huo.
“Mbinu tunazozitumia ni tofautitofauti
lakini tunaziunganisha pamoja ambazo tunaziita mkutano, kwa hiyo tunakuwa na
semina, mafundisho mbalimbali ya kiimani sambamba na mafungo,” Amesema Mangu.
Kwa upande mwingine Mangu amesema kuwa
wanapokutana wanakuwa na padri ambaye huongoza mambo yote ya kiroho lakini pia
wanakuwepo walei mbalimbali wenye historia za kiimani ambao hupewa nafasi
kufundisha.
“Mijadala mbalimbali huwepo katika
mikutano yetu ili kubadilishana uzoefu wa kiimani ikiwemo wa kiutaalamu
kulingana na kila taaluma ya kila mmoja wetu,” Amesema Mangu.
Katibu Mangu amedai kuwa katika utume
huo kipaumbele cha kwanza ni kufundishana kuelewa kuwa Mungu ndio wa kwanza na
wa mwisho katika kila jambo hapa Duniani.
“Kwahiyo taaluma na utaalamu wa mtu
haumfanyi kutokushiriki mambo ya kimungu bali kila binadamu yeyote aliyeumbwa
na Mungu anatakiwa kuanza na Mungu na
kumaliza na Mungu katika shughuli za roho na mwili.”
Aksanteeh sana Kwa kutushirikisha utume huu wa CPT
ReplyDelete