‘Mitandao ya kijamii iikomboe Tanzania’
|
WASOMI nchini wameaswa kufanya tafiti
juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii ili wabuni mbinu za matumizi sahihi ya
mitandao kuleta maendeleo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino SAUT
tawi la Dar es Salaam (Msimbazi) Padri Dk. Charles Kitima wakati akitoa
mrejesho kwa wanachuo katika kitivo cha Mawasiliano ya umma (SAUT) kuhusu
majadiliano ya usalama wa mitandao ya kijamii kati ya Tanzania na China,
uliofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.
“Mimi kama mshiriki wa majadiliano hayo na mdau wa maendeleo katika nchi
hii, mjadala uliofanyika wa kubadilishana uzoefu wa namna ya kutumia mitandao
ya kijamii kati ya Tanzania na China una manufaa endapo tutaweza kubadili
mitazamo ya namna tunavyotumia mitandao ya kijamii kwa sasa.
Ni wazi mitandao ya kijamii inasaidia kuwa na uhuru wa kujieleza kwa
maudhui yasiyopingana na sheria za nchi kwani uhuru wa kujieleza ni demokrasia
inayoleta maendeleo. Hatuwezi kukwepa matumizi ya mitandao ya kijamii kama
tunataka maendeleo. Lazima twende sambamba na teknolojia ili tusiachwe nyuma,”
Amesema Padri Kitima.
Kwa upande mwingine ameeleza kukatishwa tamaa na jamii ya kitanzania
hususani vijana ambao wanatumia mitandao ya kijamii kusambaza habari ambazo
hazijafanyiwa utafiti, uongo, uzushi na mengine.
Amewaasa wasomi nchini kusaidia kuleta mapinduzi ya matumizi sahihi ya
mitandao ya kijamii ili ilete maendeleo badala ya kulisha umma taarifa zisizo
na manufaa.
“Mjadala huu umetupa changamoto kwani wataalamu wa mitandao kutoka China
wameeleza uzoefu wa matumizi ya mitandao hii huko China wakisema kwanza
wanamiliki satelaiti na wanatumia mitandao ya kwao kama wachina na siyo
facebook, whatsApp nk.
Naibu Waziri wa Udhibiti wa mtandao wa China, Ren Xianliang amesema nchi
yao imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kudhibiti matumizi ya usalama wa
mtandao kwa kuwa walianzisha mtandao wao ambao umekua ukisaidia kufuatilia
masuala ya nchi yao vikiwamo vivutio mbalimbali ambavyo huwashawishi na kutoa
hamasa kwa wananchi wengi kuweza kutumia mtandao huo.
Amesema waziri Xianliang alisema
kuwa wao (China) katika kudhibiti matumizi ya usalama wa mitandao ya kijamii
nchini mwao wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana kuanzisha mtandao maalumu
ambapo umewasaidia kufanya vipindi mbalimbali vya kuhamasisha na kuwashawishi
wananchi kutumia mtandao huo.
“Wameweza pia kufanyia kazi ajenda za vijijini na kuleta maendeleo. Sisi
tunafanya nini? Ajenda zetu ni zipi? Tunataka nini kama taifa?
Wasomi fanyeni tafiti, leteni mawazo mapya ili tuanze safari ya maendeleo
ambayo yanawezekana kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Ni wazi hatuna satelaiti wala injini ya kwetu ambayo inaweza kutusababisha
tuwe na mitandao ya kwetu, lakini angalau tuwe na ajenda zetu za kuleta
maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu nk.
Ninakumbuka kauli ya Mwalimu Nyerere wakati aliposema katika ukumbi wa
Lumumba; ‘Wakati wenzetu wanaenda mwezini sisi twende vijijini,’ alitabiri
kuwa, ipo siku baada ya kuleta maendeleo vijijini Tanzania pia itaenda mwezini.
Sasa imefika mahali watanzania hatuwezi kuwa na maendeleo kwasababu ya
namna tunavyotumia mitandao yetu ya kijamii. Ili mradi kauli ni ya chama
tawala, mpinzani lazima apinge hata kama jambo ni la kujenga, kadhalika taarifa
au maoni ya mpinzani yawe yanajenga ama la wanachama wa chama tawala lazima
wapinge. Hali kadhalika na wafuasi wao.
Kupinga kwenyewe si kwa hoja bali hata matusi. Kuna kauli nyingi za kebehi
na uzushi kuhusu watu ambazo zinatupeleka pabaya na hatujui tunataka nini.
Wenzetu wanaunganisha miji na vijiji kutatua changamoto za maendeleo,
kutengeneza dawa, kupanua wigo wa elimu na teknolojia nyingine sisi
tunatukanana tu, tubadilike,” Amesisitiza Padri Kitima.
Amewaasa wana habari kuisaidia jamii kuchuja taarifa zinazotolewa na
watumiaji wa mitandao. Pale mtu anapotoa taarifa isiyo sahihi, mwandishi wa
habari ama wasomi katika fani mbalimbali wanaaswa watoe taarifa sahihi kwa
kutumia vielelezo vya tafiti ili kuleta mapinduzi.
Pia mitandao ya kijamii iwe ni sehemu ya kuleta maendeleo, kuwa na
mijadala wazi na huru kutoa hoja za maendeleo na mapendekezo, kuunganisha jamii
kujadili ajenda za kitaifa na kuamua kwa pamoja tufanye nini kufika kule Taifa
linapotaka.
Katika mjadala huo Serikali ya Tanzania pia imejifunza namna ya kupambana
na kuthibiti matumizi ya mitandao ya kijamii kuepusha kauli za uchochezi, chuki
nk.
Naibu Waziri wa Wizara wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin
Ngonyani amesema Serikali inajipanga kukabiliana na matumizi mabaya ya mtandao
ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wanaotumia vibaya.
Waziri Ngonyani amesema kuwa, serikali itawachukulia hatua kali wanaotumia
vibaya mitandao ya kijamii wakiwamo wanaotuma ujumbe wenye dhamira ya
kuwachafua wengine kwani Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya udhibiti wa
usalama wa matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Tanzania bado iko nyuma katika masuala ya kudhibiti usalama wa matumizi
ya mitandao kama vile Twitter, Facebook, Instagram na YouTube, wenzetu China
wamefanikiwa kudhibiti suala hilo,” amesema Mhandisi Ngonyani.
Comments
Post a Comment