MIAKA 75 YA UTUME: SI MCHEZO
Na Thomas Mambo, Tabora
HUKU Kanisa Katoliki Tanzania likiadhimisha Jubilei ya Miaka
100 ya Upadri, waamini nchini wamekumbushwa wajibu wao wa kuwa na moyo wa
shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwatoa watoto wao ili waingie katika miito ya
Upadri na Utawa na waweze kuisaidia jamii kudumisha upendo, amani, maelewano na
maendeleo.
Padri John Mungoni wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora ametoa wito
huo hivi karibuni katika Misa Takatifu ya kumpongeza Sister Maria Macktilda
Nyanzala aliyesherehekea miaka 75 ya utume wake katika Shirika la Mabinti wa
Maria Tabora.
Padri Mungoni amesema wana Itaga wanayo sababu ya kumshukuru
Mungu kwa zawadi ya Sr. Nyanzala anayetoka katika Parokia ya Itaga na kusema
waamini lazima wajitafakari na kuanza maisha mapya ya kuona kuwa Kanisa
linapata miito hiyo mitakatifu na kuachana na mazoea ya kuona wito wa ndoa ni
muhimu zaidi ya miito mitakatifu.
Aidha padri Mungoni amesema Parokia ya Itaga pia inapaswa
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mapadri wa kwanza kabisa katika Jimbo kuu
Katoliki Tabora, yaani Pd. Raphael Luziga, Pd. Raphel Kavula na Pd. Simon
Kakurumo ambao wote ni marehemu.
Ameongeza kuwa mapadri na watawa wanaishi maisha yao wakimshuhudia
Kristo hapa Duniani, hivyo wazazi waandae mazingira rafiki kwa watoto wao
kuingia seminarini na nyumba za malezi.
Sr. Nyanzala alizaliwa mwaka 1919 katika kijiji cha Masagala
Manispaa ya Tabora na baadaye alianza safari yake ya kumfuata Kristo kwa kupata
Sakramenti za Kanisa ambapo alijiunga na nyumba ya malezi Usongo Jimbo Kuu Tabora
mwaka 1940.
Pamoja na wito wa Utawa alijiendeleza katika fani ya Uuguzi,
fani ambayo ilimsaidia katika kuhudumia watu mbalimbali wenye shida ya afya.
Comments
Post a Comment