Mashahidi wa Uganda walisimama kidete kulinda imani na kutetea maadili


Namgongo ni mahali ambapo mashuhuda wa imani kutoka Uganda waliyamimina maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake, hija ya mateso iliyoanzia Munyonyo na kuhitimishwa hapo tarehe 3 Juni 1886 na kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu hapo tarehe 18 Oktoba 1964. Hili ni eneo ambalo limebahatika kutembelewa na Mwenyeheri Paulo VI,  Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Francisko. Mashuhuda wa imani nchini Uganda wamekuwa kweli ni chemchemi ya miito mitakatifu ya Upadre na Utawa, kwani imeongezeka maradufu nchini Uganda. Ibada kwa Mashahidi wa Uganda imeenea sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, kuna: Makanisa na taasisi ambazo zimewateua Mashahidi wa Uganda kuwa wasimamizi wao pamoja na kuongezeka kwa utume wa wamini walei nchini Uganda. Mashuhuda wa imani wamefungua kurasa mpya za maisha na utume wa Kanisa nchini Uganda na Afrika katika ujumla wake.
Afrika inasimama na imekombolewa kwa damu ya mashuhuda wa imani kiasi kwamba, kwa sasa Bara la Afrika limekuwa ni nyumba ya Injili na maskani mapya ya Yesu. Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linaishukuru Serikali kwa kuamua kwamba, tarehe 3 Juni ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Mapumziko ili kuwaenzi Mashahidi wa Uganda, tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha yao ya kila siku. Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuambata ukweli, ili kuondokana na maovu jamii pamoja na mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho yanayoendelea kuzagaa duniani utadhani umande wa asubuhi. Mahali ambapo hakuna ukweli, watu wanajikuta wanatumbukia katika maovu jamii na hivyo kushindwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli ambao unawapaswa kuwaweka huru kama anavyosema Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu. Hii ni changamoto pia kwa waamini kuachana na mtindo wa maisha ya ndumilakuwili, mchana wanaonekana kuwa ni Wakristo wema na wachamungu, usiku wanageuka kuwa ni wapagani kana kwamba, hawajawahi kuingia hata siku moja Kanisani.
Matokeo yake ni kuendekeza imani za kishirikina ambazo zimekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa haki msingi za binadamu na maafa katika jamii nyingi. Hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Mashahidi wauganda Namgongo, iwe ni fursa kuwa kweli ni mashuhuda wa imani na vyombo vya huruma na mapendo yanayomwilishwa katika imani tendaji. Familia ya Mungu nchini Uganda itambue kwamba, nguvu yake inafumbatwa katika imani ya Mashahidi wa Uganda kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Uganda, mwaka 2015. Mashahidi wa Uganda walisimama kidete, kulinda na kutetea ukweli wa kiimani na kiimadili kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, Mashahidi wa Uganda waliouwawa kwa amri ya Kabaka Mwanga wa Pili walikuwa ni 45 na kati yao Wakatoliki walikuwa ni 22, waliouwawa kati ya mwaka 1885 na mwaka 1887 kwa kuchomwa moto wakiwa hai!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI