Zaidi ya Vijana 6,000 wanufaika na mafunzo ya maadili Arusha

n  Na Doreen Aloyce, Arusha

ZAIDI ya vijana wakatoliki elfu sitini (6000) wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha wamenufaika na elimu ya malezi  na maadili mema ambayo itawawezesha wawe na utu na kuboresha mbegu bora katika familia.
Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya sherehe ya upadrisho wa mapadri watatu zilizofanyika katika parokia ya Burka Arusha.
Askofu Lebulu amebainisha kuwa Jimbo hilo linapenda kuwaandaa viongozi wakiwa wadogo kupitia shule za pekee za Seminari za Jimbo hilo ikiwemo ya Usa River ambayo ni kwa ajili ya wavulana pamoja na ya Seminari iliyopo Kisongo ambayo ni ya kuwaandaa wasichana ili waweze kukua katika maadili mema.
Amefafanua kuwa vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinazidi kushamiri katika jamii kutokana na wazazi kushindwa kusimamia malezi ya watoto na kwamba Kanisa Katoliki limejiwekea utaratibu wa kuelimisha vijana ambao wamemaliza darasa la saba ili kuwajengea maadili ambayo yatawajenga katika utu na hatimaye kuwezesha familia kujua.
Padri Fulgence Mallya ambaye ni Mkurugenzi wa Miito wa Jimbo hilo amesema kuwa kupatikana kwa mapadri hao ni neema kwani awali ilikuwa changamoto na kwamba wataweza kulisaidia Kanisa Katoliki kufikia watu wengi na kuwapatia huduma.
Amesema kuwa Jimbo hilo limekaa miaka mitano bila kupata watumishi na kwamba kufanikiwa  kupata mapadri watatu  katika Jimbo kutasaidia  Parokia kuongezeka na kupata wahudumu pia kuweza kuwafikia watu wanaohitaji huduma katika jamii tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
“Jimbo letu limekaa muda wa miaka mutano bila kupata mapadri wapya, hivyo naamini mapadri hawa wataweza kuhudumia parokia zetu lakini hata kuweza kuhudumia watu kwani watu nao wanazidi kuongezeka lakini watenda kazi ni wachache zaidi,” Amesema.
Aidha amesema kuwa wakristo wanapaswa kuendelea kusali kumwomba Mungu ili zile mbegu  ya wito zinazosiwa na Mungu  katika familia ziendelee kukua na hatimaye waendelee kupata mapadri ambao watawezesha  kubadilisha ulimwengu kuwa na maadili mema.
Amewataja mapadri waliopewa daraja hilo kuwa ni pamoja na padri Alfred Fadhili (anakwenda kutumika Seminari ndogo ya Jimbo Oldonyosambu), padri Kariuki Ndege (anakwenda Parokia ya Kijungu Wilaya ya Kiteto)  na  padri Emanueli Swai (amepangiwa Seminari ya matayarisho User River ya Mtakatifu Kaloli Rwanga).


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU