MIAKA 75 YA UTUME: SI MCHEZO



Na Thomas Mambo, Tabora
HUKU Kanisa Katoliki Tanzania likiadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Upadri, waamini nchini wamekumbushwa wajibu wao wa kuwa na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwatoa watoto wao ili waingie katika miito ya Upadri na Utawa na waweze kuisaidia jamii kudumisha upendo, amani, maelewano na maendeleo.
Padri John Mungoni wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora ametoa wito huo hivi karibuni katika Misa Takatifu ya kumpongeza Sister Maria Macktilda Nyanzala aliyesherehekea miaka 75 ya utume wake katika Shirika la Mabinti wa Maria Tabora.
Padri Mungoni amesema wana Itaga wanayo sababu ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Sr. Nyanzala anayetoka katika Parokia ya Itaga na kusema waamini lazima wajitafakari na kuanza maisha mapya ya kuona kuwa Kanisa linapata miito hiyo mitakatifu na kuachana na mazoea ya kuona wito wa ndoa ni muhimu zaidi ya miito mitakatifu.
Aidha padri Mungoni amesema Parokia ya Itaga pia inapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mapadri wa kwanza kabisa katika Jimbo kuu Katoliki Tabora, yaani Pd. Raphael Luziga, Pd. Raphel Kavula na Pd. Simon Kakurumo ambao wote ni marehemu.
Ameongeza kuwa mapadri na watawa wanaishi maisha yao wakimshuhudia Kristo hapa Duniani, hivyo wazazi waandae mazingira rafiki kwa watoto wao kuingia seminarini na nyumba za malezi.
Sr. Nyanzala alizaliwa mwaka 1919 katika kijiji cha Masagala Manispaa ya Tabora na baadaye alianza safari yake ya kumfuata Kristo kwa kupata Sakramenti za Kanisa ambapo alijiunga na nyumba ya malezi Usongo Jimbo Kuu Tabora mwaka 1940.
Pamoja na wito wa Utawa alijiendeleza katika fani ya Uuguzi, fani ambayo ilimsaidia katika kuhudumia watu mbalimbali wenye shida ya afya.





Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU