‘Mitandao ya kijamii iikomboe Tanzania’


n  Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam

WASOMI nchini wameaswa kufanya tafiti juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii ili wabuni mbinu za matumizi sahihi ya mitandao kuleta maendeleo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino SAUT tawi la Dar es Salaam (Msimbazi) Padri Dk. Charles Kitima wakati akitoa mrejesho kwa wanachuo katika kitivo cha Mawasiliano ya umma (SAUT) kuhusu majadiliano ya usalama wa mitandao ya kijamii kati ya Tanzania na China, uliofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.
“Mimi kama mshiriki wa majadiliano hayo na mdau wa maendeleo katika nchi hii, mjadala uliofanyika wa kubadilishana uzoefu wa namna ya kutumia mitandao ya kijamii kati ya Tanzania na China una manufaa endapo tutaweza kubadili mitazamo ya namna tunavyotumia mitandao ya kijamii kwa sasa.
Ni wazi mitandao ya kijamii inasaidia kuwa na uhuru wa kujieleza kwa maudhui yasiyopingana na sheria za nchi kwani uhuru wa kujieleza ni demokrasia inayoleta maendeleo. Hatuwezi kukwepa matumizi ya mitandao ya kijamii kama tunataka maendeleo. Lazima twende sambamba na teknolojia ili tusiachwe nyuma,” Amesema Padri Kitima.
Kwa upande mwingine ameeleza kukatishwa tamaa na jamii ya kitanzania hususani vijana ambao wanatumia mitandao ya kijamii kusambaza habari ambazo hazijafanyiwa utafiti, uongo, uzushi na mengine.
Amewaasa wasomi nchini kusaidia kuleta mapinduzi ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili ilete maendeleo badala ya kulisha umma taarifa zisizo na manufaa.
“Mjadala huu umetupa changamoto kwani wataalamu wa mitandao kutoka China wameeleza uzoefu wa matumizi ya mitandao hii huko China wakisema kwanza wanamiliki satelaiti na wanatumia mitandao ya kwao kama wachina na siyo facebook, whatsApp nk.
Naibu Waziri wa Udhibiti wa mtandao wa China, Ren Xianliang amesema nchi yao imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kudhibiti matumizi ya usalama wa mtandao kwa kuwa walianzisha mtandao wao ambao umekua ukisaidia kufuatilia masuala ya nchi yao vikiwamo vivutio mbalimbali ambavyo huwashawishi na kutoa hamasa kwa wananchi wengi kuweza kutumia mtandao huo.
Amesema waziri Xianliang  alisema kuwa wao (China) katika kudhibiti matumizi ya usalama wa mitandao ya kijamii nchini mwao wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana kuanzisha mtandao maalumu ambapo umewasaidia kufanya vipindi mbalimbali vya kuhamasisha na kuwashawishi wananchi kutumia mtandao huo.
“Wameweza pia kufanyia kazi ajenda za vijijini na kuleta maendeleo. Sisi tunafanya nini? Ajenda zetu ni zipi? Tunataka nini kama taifa?
Wasomi fanyeni tafiti, leteni mawazo mapya ili tuanze safari ya maendeleo ambayo yanawezekana kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Ni wazi hatuna satelaiti wala injini ya kwetu ambayo inaweza kutusababisha tuwe na mitandao ya kwetu, lakini angalau tuwe na ajenda zetu za kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu nk.
Ninakumbuka kauli ya Mwalimu Nyerere wakati aliposema katika ukumbi wa Lumumba; ‘Wakati wenzetu wanaenda mwezini sisi twende vijijini,’ alitabiri kuwa, ipo siku baada ya kuleta maendeleo vijijini Tanzania pia itaenda mwezini.
Sasa imefika mahali watanzania hatuwezi kuwa na maendeleo kwasababu ya namna tunavyotumia mitandao yetu ya kijamii. Ili mradi kauli ni ya chama tawala, mpinzani lazima apinge hata kama jambo ni la kujenga, kadhalika taarifa au maoni ya mpinzani yawe yanajenga ama la wanachama wa chama tawala lazima wapinge. Hali kadhalika na wafuasi wao.
Kupinga kwenyewe si kwa hoja bali hata matusi. Kuna kauli nyingi za kebehi na uzushi kuhusu watu ambazo zinatupeleka pabaya na hatujui tunataka nini. Wenzetu wanaunganisha miji na vijiji kutatua changamoto za maendeleo, kutengeneza dawa, kupanua wigo wa elimu na teknolojia nyingine sisi tunatukanana tu, tubadilike,” Amesisitiza Padri Kitima.
Amewaasa wana habari kuisaidia jamii kuchuja taarifa zinazotolewa na watumiaji wa mitandao. Pale mtu anapotoa taarifa isiyo sahihi, mwandishi wa habari ama wasomi katika fani mbalimbali wanaaswa watoe taarifa sahihi kwa kutumia vielelezo vya tafiti ili kuleta mapinduzi.
Pia mitandao ya kijamii iwe ni sehemu ya kuleta maendeleo, kuwa na mijadala wazi na huru kutoa hoja za maendeleo na mapendekezo, kuunganisha jamii kujadili ajenda za kitaifa na kuamua kwa pamoja tufanye nini kufika kule Taifa linapotaka.

Katika mjadala huo Serikali ya Tanzania pia imejifunza namna ya kupambana na kuthibiti matumizi ya mitandao ya kijamii kuepusha kauli za uchochezi, chuki nk.

Naibu Waziri wa Wizara wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani amesema Serikali inajipanga kukabiliana na matumizi mabaya ya mtandao ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wanaotumia vibaya.
Waziri Ngonyani amesema kuwa, serikali itawachukulia hatua kali wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii wakiwamo wanaotuma ujumbe wenye dhamira ya kuwachafua wengine kwani Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya udhibiti wa usalama wa matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Tanzania bado iko nyuma katika masuala ya kudhibiti usalama wa matumizi ya mitandao kama vile Twitter, Facebook, Instagram na YouTube, wenzetu China wamefanikiwa kudhibiti suala hilo,” amesema Mhandisi Ngonyani.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU