Jeshi la Polisi latakiwa kumkamata mtuhumiwa wa ubakaji


n Na Dotto Kwilasa, Dodoma

BAadhi ya wakazi wa mkoa wa Dodoma wameliomba Jeshi la Polisi mkoani hapa kudhibiti vitendo vya uhalifu wa kijinsia ambavyo vimekuwa vikitokea mara kwa mara.
Hatua hii imekuja baada ya mfanyabiashara wa mtaa wa Swaswa Kata ya Ipagala Manispaa ya Dodoma Charles Kalinga maarufu kama Chaz Pub mwenye umri wa miaka 43  kutuhumiwa kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17 wa kidato cha nne katika  Shule ya Sekondari ya Dodoma.
Tukio hilo limetokea hivi karibuni majira ya saa moja usiku katika mtaa huo wa Swaswa baada ya mtoto huyo kusikika akipiga kelele akiwa katika pagale ambapo mama wa mtoto na majirani walimkuta mtuhumiwa akiwa amemlalia mtoto huyo huku akiwa ameshamuingilia kimwili.
Akiongea kwa niaba ya wananchi wenzake, Bi Devota Metusela amesema wamechoshwa na vitendo hivyo vinavyojirudia na kusababisha hofu kwa jamii.
“Kwa kweli hali hii inatuchosha mpaka wakati mwingine tunakosa imani na Jeshi la Polisi,” Anasema.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt Caroline Damiani amethibitisha kumpokea mwanafunzi huyo ambaye anadaiwa kubakwa ambapo alikuwa na hali mbaya.
Pia Dkt Caroline amesema wamempokea  mgonjwa Charles Kalinga ambaye anashukiwa juu ya ubakaji huo akiwa na majeraha ambapo ametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Naye Balozi wa Mtaa wa Kidongochekundu, Rojas Mtunya amesema kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na tabia ya kufanya vitendo vya ubakaji mara kwa mara na hivyo kuliomba jeshi la polisi kutenda haki.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Dodoma siyo salama kwa wahalifu na hivyo lazima sheria ichukue mkondo wake.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU