MIAKA 21 REDIO MARIA TANZANIA YAFANA, PINDA ATOA RAI KWA WAAMINI

Viongozi wa Dini nchini wameshauriwa kutazama kwa kina mafundisho wanayoyatoa kwa waamini wao, hasa kwa wakati huu ambao dunia imemezwa na Utandawazi,  kwa kuyaelekeza zaidi katika kuamsha ari mpya ya kuokoa kizazi kijacho ambacho ni vijana na watoto, ambao wengi wao pia wamemezwa na mmomonyoko wa maadili.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mizengo Pinda, wakati akiongoza maadhimisho ya Miaka 21 ya Uinjilishaji wa Redio Maria hapa nchini Tanzania, yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki Mbeya.
Waziri Mkuu Mstaafu Pinda akiongelea suala zima la mmomonyoko wa maadili ambalo linaonekana kuwameza vijana wengi, amesema hali iliyopo sasa si alama nzuri kwa Kanisa la kesho, ambalo linategemea miito mitakatifu kutoka kwa kizazi hiki cha sasa, ambacho kinaonekana kumezwa zaidi na malimwengu na kujiweka nyuma katika masuala ya Imani.
Akitolea mfano ushiriki wa Jumuiya ndogondogo, amesema kuwa vijana wengi na watoto hawahudhurii huko, ikiwemo pia ushiriki wao kwa mambo ya Kanisa ni wakusuasua, huku akitolea mfano kwenye familia yake ambayo anaishi na vijana wengi, “Mfano pale nyumbani kwangu na Mama Pinda tunalea vijana wengi mno lakini katika suala la kusali na kwenda Jumuiya ni wazito sana, ikitokea tunawalazimisha kusali pamoja usiku sala wanazo sali nyingi hazina tafakari (meditation) na mara nyingi zinakuwa za harakaharaka, hali ambayo ni tofauti na unapowakuta wakiwa wanatizama luninga, kucheza game,au namna wanavyutumia muda mwingi katika simu zao za mkononi,” Amesema Pinda.
Aidha, amezikumbusha familia za kikristo kila moja kurejesha ule utamaduni wa zamani wa kusali pamoja usiku hasa sala ya Rozari Takatifu, sambamba na kuwafundisha watoto na vijana kusali kwa kutafakari, huku akizitaka familia kutokujisahau kwa kumezwa na majukumu na kusahau suala la malezi kwa familia zao, ikiwa ni pamoja na kuzungumza na kula pamoja nao hasa siku za mwisho wa juma na zaidi jumapili na siku nyingine za mapumziko.
Kwa upande wa redio Maria Tanzania, Waziri Mkuu Mstaafu ameishauri redio hiyo kuhakikisha kwamba inaandaa vipindi vyenye kuelimisha jamii kiimani, hasa kutoa mafunzo yanayoelekeza kuondokana na imani za kishirikina ambazo bado zipo katika jamii ya watanzania wa leo, ambapo akatolea mfano mauaji ya Albino,”Padri Maendeleo na timu yako nawashauri mjikite pia katika kutoa mafundisho yanayoelekeza watu kuondokana na dhana ya ushirikina, na badala yake muwaelekeze katika kufanya kazi kwa bidii na kuishi kwa kumtegemea Mungu zaidi,” amesema Pinda.
Aidha hakusita kuwasisitiza waandaaji wa vipindi kwenye redio za Kanisa kujitika zaidi katika kuandaa vipindi vingi vinavyojenga maadili kwa vijana, kwa lengo la kuimarisha miito na kujenga taifa lenye watu wanaofuata maadili hata katika kuwatumikia wanajamii, na vitakavyowajengea uaminifu katika imani yao hivyo wataondokana na dhana mbovu iliyopo kwa wakati huu ya waamini kuhama makanisa kila kukicha kwa lengo la kutafuta miujiza na vitakavyowafanya walipende Kanisa na wajisikie fahari kulitumikia.
Wakati huo huo, Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evarist Markusi Chengula I.M.C, aliyeongoza ibada ya misa Takatifu ya kilele cha maadhimisho ya miaka 21 ya  redio Maria Tanzania, amewashukuru viongozi wa redio hiyo akiwemo Rais Julius Kira na Mkurugenzi Padri John Maendeleo CSSp, kwa kupeleka maadhimisho hayo jimboni kwake, ambayo yamemfanya aweze kukaa meza moja na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya mkoa ambao hajawahi kukutana nao na kuzungumza nao kwa kipindi chote cha uongozi wake kama Askofu wa Jimbo hilo.
Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 21 ya Uinjilishaji wa redio Maria Tanzania tangu kuanzishwa kwake, kilifanyika Julai 2 mwaka huu, ambapo katika maadhimisho hayo aliyekuwa mgeni rasmi Mh Pinda aliongoza harambee ya kuiwezesha redio hiyo na zilipatikana jumla ya shilingi milioni 25, ahadi zikiwa ni shilingi 13,128,000 na pesa taslimu zikiwa ni shilingi 11,872,000.
Hata hivyo maadhimisho hayo yalitanguliwa na Hija ya kiroho ya siku 5 kwa mahujaji waliotoka katika majimbo Makuu ya Songea, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, pamoja na majimbo ya Zanzibar, Singida, Moshi, Iringa, Mpanda, Mtwara, Ifakara, Mbinga wakiwemo wenyeji Jimbo Katoliki Mbeya, walitembelea katika maeneo mbalimbali likiwemo Kanisa la Hija Mwanjelwa, kupanda mlima wa Hija Loleza, kutembelea daraja la Mungu na kushiriki mafundisho ya kiroho toka kwa mapadri mbalimbali wa Jimbo Katoliki Mbeya akiwemo Padri Anthon Makunde aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania miaka ya nyuma.





















Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU