Wanawake waomba Sheria ya Ardhi itafsiriwe kwa kiswahili

n Na Dotto Kwilasa, Dodoma.

WANAWAKE nchini wameiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutafsiri sheria mbalimbali ikiwemo ya ardhi kwa lugha ya Kiswahili na kutoa elimu hiyo ili kuwasaidia  wanawake wa vijijini ambao wamekuwa wakikosa haki zao kwa kutokujua sheria hizo.
Hatua hii imekuja baada ya wanawake wengi kulalamika kudhulumiwa ardhi na baadhi ya viongozi wa vijiji huku wakiachwa bila malipo hali inayowadidimiza kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Afisa habari wa Jukwaa la wakulima wanawake wa Tanzania Melea Sulutya wakati akisoma risala katika Kongamano la wanawake lilioandaliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali linalosaidia vikundi vya wakulima (Action Aid) katika Kijiji cha Mloda Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.
Sulutya amesema kutokuzielewa sheria zinazomlinda mwanamke hasa katika masuala ya kumiliki ardhi kumefanya wanawake wengi kuendelea kuishi katika manyanyaso bia kujua jinsi ya kudai haki zao.
Wakati huo huo mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) mkazi wa kijiji cha Buigiri amesema wanawake wanadharauliwa kiasi kinachowafanya kukutana na ugumu wa maisha huku akitumia nafasi hiyo kuomba msaada wa sheria juu ya kesi yake ya kubakwa ambayo mtuhumiwa alipewa hukumu ya kulipa faini ya shilingi laki tatu ambayo haiendani na kosa alilofanya.
“Nilibakwa na mwanaume ambaye mpaka sasa naishi naye kijiji kimoja, kitu hiki kinaniumiza sana..mtu amebaka halafu anatozwa faini ya shilingi laki tatu!moyo wangu unaniuma sana kwa kuwa najua hali hii ikiendelea hivi wanawake wengi watazidi kubakwa,”amesema mwanamke huyo.
Naye Mratibu uwezeshaji umma kifedha katika sekta ya kilimo (Action Aid)   Joram Wimmo amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 asilimia 30 ya wanawake wawe wanamiliki ardhi na kuzalisha katika ardhi hizo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Elias Wilson amesema kuwa ni jukumu la Halmashauri kuhakikisha vikundi vinavyoanzishwa na wahisani vinaendelezwa na kuwasaidia wananchi wengi zaidi.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU