Jamii yaaswa kuwathamini watoto yatima

n  Na Thompson Mpanji, Mbeya

MKURUGENZI wa utume wa Walei Jimbo Katoliki Mbeya na vyama vya Mashirika na Jumuiya za Kitume Jimbo, Padri Sirilo Mwalyoyo ameyaalika Mashirika  na wadau mbalimbali  wa masuala ya kijamii kushirikiana na Serikali katika kuwalinda na kutetea haki za watoto yatima  na wanaoishi katika mazingira hatarishi  ili waweze kukua katika malezi  na maadili mema.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea kituo cha watoto yatima cha Aman kilichopo Kata ya Nsalaga jijini Mbeya, ziara  iliyoratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la Sauti ya Mama Afrika(SAMAFO) na watu wenye mapenzi mema, padri Mwalyoyo amesema kuwa  binadamu wanapoteza dhana  ya utu  na hivyo kuwasihi wasamaria wema  kuwajali, kuwasaidia  na kuwaendeleza  watoto yatima ili waweze kujisikia kuwa nao ni binadamu kama walivyo wengine.
“Watu ambao hawana usaidizi wa karibu wanayo haki ya kuishi, na kwa vile hawana haki ya kujitetea  basi wale wanaowalinda waweze kuwatetea na kuwalinda dhidi ya ukatili wa aina yoyote  ile na  hatimaye  waweze kuwa na faida kwa jamii na Taifa.”
Padri Mwalyoyo amefafanua  kuwa  watoto yatima  ni jamii inayohitaji msaada katika nyanja mbalimbali za makuzi mathalani mavazi mazuri, malazi mazuri, elimu na afya na kwamba jukumu hili ni vyema libebwe  kwa ukaribu na watu wenye nafasi badala ya kuiachia Serikali, makanisa na misikiti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji  wa SAMAFO, Tabitha Bughali  ameiomba Serikali  iwapatie uwanja watakaojenga nyumba ya amani  ambayo lengo kuu ni kuwahifadhi na kuwakutanisha  wanawake, vijana na watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili katika jamii wanazoishi na vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo misaada ya kisheria.
Aidha amewaonya watoto hao kutojihusisha na masuala ya anasa za kidunia  ambazo mwisho wake zitawasababisha kupoteza maisha, kufanyiwa ukatili, kupewa mimba na kutelekezwa na mwisho kuzitoa ama kutupa watoto huku akiwasihi watoto hao kuwa watakapomuona mwenzao anakengeuka basi walindane wenyewe kwa  wenyewe kwa kutoa taarifa kwa  wasimamizi wa kituo ama wamtafute na kumshirikisha yeye.
Msimamizi wa kituo  hicho, Bahati Pangani amewashukuru  wasamaria wema kuwatembelea, kufurahi na kula nao pamoja  ikiwemo na kuwapatia mahitaji mbalimbali kwani ndicho kitu pekee wanachokihitaji katika maisha yao na kwamba  kwa mujibu wa maelekezo wa Serikali watoto hao  wanaishi katika jamii zao na kukutana  walau mara mbili  kwa wiki katika siku za Jumamosi na Jumapili.
Hata  hivyo  mmoja wa wahudumu  wa kujitolea kutoka nchini Uswisi, Anna Sprecher ameelezea furaha yake baada ya kuiona jamii ya kitanzania inavyowajali watoto yatima, kuwatembelea na kuwapatia misaada mbalimbali ikiwemo ya kielimu na kisheria  ambayo itawasaidia katika maisha yao ya baadaye na hatimaye kuwakumbuka yatima wenzao pia.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU