Tumieni vipaji vyenu kwa faida-Askofu Ruzoka asisitiza

n  Na Thomas Mambo, Tabora.
ASkofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora Mhashamu Paulo Ruzoka amewataka waamini wote kujitegemeza kwa Mwenyezi Mungu katika kutumia vipaji vyao kwa faida ya wote popote walipo bila majivuno.
Rai hiyo ameitoa hivi karibuni katika Misa Takatifu aliyoiadhimisha katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, Tabora.
Katika mahubiri yake Askofu Mkuu Ruzoka amesema ili padri afanikiwe katika utume wake hana budi kujitegemeza kwa Kristo mwenyewe na kuwa tayari kutumia karama zake kwa faida ya wote.
Akirejea maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo, (Lk 10:1-9 ), Askofu Mkuu amesema hata Bwana wetu Yesu kristo aliwatuma wawili wawili baada ya kuwafunda na wao kuwa tayari kujitegemeza kwake .
Ndani ya Misa hiyo Takatifu , Daraja ya Upadri ilitolewa kwa Shemasi Ignas Gerald Akilimali wa Parokia ya Mt. Teresia  wa Mtoto Yesu. Akimuasa Shemesi huyo amesema padri ni mhudumu wa Hekalu la Bwana hivyo anapaswa kujitoa mzima kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.
“Padri katika utume wake hana budi kuishi roho ya upendo, na kwa kufanya hivyo anawafanya watu walio chini yake wampende Mwenyezi Mungu.” Amesema.
Pia Askofu Mkuu Ruzoka amewaasa mapadri wote kutekeleza utume wao kwa upendo, unyenyekevu na moyo wa shukrani.
“Mapadri waige mfano wa mwito wa Kristo kuwa na busara wanapotekeleza majukumu yao kwani yapo maeneo watapokelewa na mazingira, mengine watakataliwa hivyo wasikate tamaa.”
Aidha Askofu Mkuu amebainisha kuwa shabaha kuu ya padri iwe ni kuwafikisha watu mbinguni na si vinginevyo.
Askofu Mkuu amewashukuru wazazi wa padri na wote ambao watoto wao ni mapadri na watawa kwa kumpa Mungu zawadi ya thamani.  Pia amewaomba wakristo wote kuendelea kuombea miito mitakatifu ya upadri na utawa ili Kanisa lisipungukiwe wahudumu.
Waamini wamemuunga mkono Askofu Mkuu Ruzoka kwa kumzawadia padri Ignas Akilimali gari dogo aina ya Rav 4 lenye thamani ya shilingi milioni 12 na nusu pesa za kitanzania.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU