‘Anayemtangaza Mungu hawezi kusambaza habari mbaya’ Ask Nzigilwa


n  Na Pascal Mwanache, Dar es salaam

KANISA linapojiandaa kuadhimisha Siku ya Upashanaji Habari, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam amesema kuwa jamii inayofurahia kusambaza habari mbaya kamwe haimtangazi Mungu. Amesema hayo hivi karibuni katika Misa ya shukrani kwa jubilei ya miaka 25 ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, tangu aliongoze jimbo hilo.
Askofu Nzigilwa amesema kuwa waamini hawana budi kupokea habari njema na kuzipeleka kwa watu, licha ya ukweli kwamba habari njema huwa hazipendwi na watu.
“Watu wanapenda kusikia habari za ovyo. Kutopenda habari njema ni kikwazo katika kumtangaza Mungu, hivyo kila mmoja awe msaada katika uinjilishaji na siyo kuwa kikwazo. Pia msiwe sababu ya watu kuumia wanapoleta habari njema, kabla ya kuitangaza habari njema tuwe tayari kuipokea kwanza” ameeleza.
Kanisa linajiandaa kuadhimisha siku ya upashanaji habari hapo Agosti 6, ambapo Kurugenzi ya Mawasiliano Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) itaadhimisha siku hiyo kwa Misa Takatifu, maonyesho ya kazi inazozifanya na kisha mada mbalimbali, ambapo maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika TEC Kurasini jijini Dar es salaam.
Baadhi ya kazi zitakazoonyeshwa katika maadhimisho hayo ni pamoja na studio mpya na ya kisasa inayotarajiwa kuanza kukodishwa kwa ajili ya kuzalisha vipindi mbalimbali, uzalishaji wa gazeti la Kiongozi, uchapishaji wa vijarida, kalenda, kadi na ubunifu unaofanywa katika kitengo cha usanifu.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Fransisko katika maadhimisho ya siku ya Upashanaji Habari unaongozwa na kauli mbiu “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe” (Is 43:5), ambapo ametoa wito kwa vyombo vya habari kutangaza habari za matumaini na imani badala ya kujikita katika kutangaza habari mbaya, za ovyo na zenye kukatisha tamaa.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU