Kilele Jubilei miaka 100 upadri Tz

Zaidi ya 3000 kushiriki Dodoma

n  Na Pascal Mwanache, Dar

IMEELEZWA kuwa zaidi ya mapadri 1000, walei 1000 na watawa 1000 wanatarajiwa kushiriki maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya Miaka 100 ya Upadri Tanzania, yanayotarajiwa kufanyika katika Jimbo Kuu Katoliki Dodoma mnamo Agosti 15, 2017.
Akiongea na Kiongozi hivi karibuni, Katibu wa Umoja wa Mapadri Tanzania (UMAWATA) Padri Jovitus Mwijage ametoa wito kwa mapadri, watawa na walei kujitokeza na kuthibitisha ushiriki wao katika maadhimisho hayo, kwa kulipia mchango wa shilingi 200,000/= ambapo itawawezesha kushiriki kilele hicho kuanzia Agosti 13 hadi 16.
Akielezea ratiba ya maadhimisho hayo, Padri Mwijage amesema kuwa washiriki wanatarajiwa kuwasili Dodoma Agosti 13 ambapo Misa ya ufunguzi itafanyika Agosti 14 kuanzia saa 2 asubuhi katika Kanisa Kuu la jimbo. Baada ya Misa Takatifu washiriki watapata fursa ya kushiriki semina ambapo mapadri watakuwa katika eneo lao huku waamini na watawa nao wakipatiwa semina hiyo katika eneo jingine.
“Semina ya kwanza kwa mapadri itatolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Desderius Rwoma, na mada inasema ‘Sababu zinazoweza kusaidia upatikanaji wa miito kwa haraka. Mada ya pili itahusu ‘baada ya miaka 100 ya upadri, maisha yetu ya kiroho, mahusiano yetu kama mapadri na utume wetu uweje’ na mada hii itatolewa na Padri Titus Amigu” amesema.
Ameongeza kuwa katika kuelekea kilele hicho mapadri katika majimbo mbalimbali nchini wameshiriki katika kuzindua jubilei hiyo kijimbo pamoja na hija zilizolenga kuwaimarisha mapadri hao. Amesema kuwa Januari 24 hadi 28, 2017 mapadri walihudhuria semina iliyofanyika katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambapo majimbo mbalimbali yalituma wawakilishi.
“Lengo la semina na hija mbalimbali zilizofanyika ni kupyaisha utume wa mapadri baada ya miaka 100 ya upadri. Tulifanya pia semina ya wakufunzi wa seminari za jimbo ambayo iliwakutanisha magombera wa seminari kubwa na ndogo na baadhi ya wakufunzi na wakurugenzi wa miito majimboni” amesema.
Pia ameeleza kuwa yeyote anayehitaji kushiriki maadhimisho hayo huko Dodoma anapaswa kutuma fedha za mchango na jina lake kwenye akaunti za UMAWATA au kwa kuwasiliana na wenyeviti wa umoja huo walioko majimboni au kwa kupiga namba 0765746644.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU